Lumbanga: Tusiogope mapya kwenye Katiba

KATIBU Mkuu Kiongozi wa zamani, Balozi Dk Matern Lumbanga (76) amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kukubali kuanza kwa mchakato wa mabadiliko ya Katiba ya Tanzania.

Dk Lumbanga alisema hayo alipozungumza na waandishi wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) nyumbani kwake Masaki, Dar es Salaam hivi karibuni.

Alisema Katiba ya sasa si mbaya lakini kuna vitu vingi vinahitaji marekebisho hivyo, Rais Samia amefanya jambo jema kuruhusu mchakato wa mabadiliko ya sheria mama ya nchi.

“Katiba yetu ilikuwa nzuri pale ilipotungwa na imeendelea na uzuri huo, sasa umekuwa overtaken by time (umezidiwa na mahitaji ya sasa). Lazima sasa tukubali kuleta mabadiliko machache kwa maana ya kuiboresha,” alisema Dk Lumbanga na kuongeza:

“Kwa hiyo uzoefu wa kipindi fulani usiwe ndio pingamizi la mambo mapya. Kama kuna mawazo mapya tuyatafakari, yale mazuri tuyajumuishe katika Katiba yetu, kama hayatufai basi hayatufai.”

Alisema Tanzania si kisiwa hivyo lazima iwe tayari kuyapokea mabadiliko na kuwasaidia watu wake kuwaelekeza kwenye mwelekeo sahihi kwa manufaa ya nchi.

Dk Lumbanga akasifu uwazi wa Rais Samia kwenye suala la Katiba na akasema muda unabadilika hivyo ni muhimu kukubali mabadiliko yenye lengo la kuboresha.

Akatoa mfano vijana wenye umri wa miaka 30 au chini ya hapo hivyo hawakuwepo wakati Katiba ya sasa inatungwa.

“Wote hawa hawana ideas (mawazo) kweli? Kwa hiyo ni vizuri tukaendelea ku-accommodate some necessary changes (kujumuisha mabadiliko ya lazima) za kwenda na wakati na ninaposema kwenda na wakati simaanishi kwamba sisi tuliokuwepo tumepitwa na wakati hapana,” anasema Dk Lumbanga na kuongeza:

“Nadhani watu wote wenye nia njema na nchi hii watafurahi, wacha watu watoe madukuduku yao na nini, at the end of the day (hatimaye) tuwe na katiba ambayo yenye madukuduku machache kuliko kung’ang’ania tu kusema huwezi kusahihisha hata koma.”

Historia inaonesha Katiba ya sasa ya mwaka 1977 imefanyiwa mabadiliko mara 14 katika nyakati tofauti kuanzia mwaka 1979 hadi 2005.

Safari ya kusaka Katiba mpya Tanzania ilianza mwaka 2012 wakati Tume ya Jaji, Joseph Warioba ilipoanza kukusanya maoni.

Tume iliandika Rasimu ya Katiba ambayo baada ya kujadiliwa na Bunge la Katiba ikaandaliwa Katiba Pendekezwa ya Tanzania.

Januari 3, mwaka huu, Rais Samia Suluhu Hassan aliridhia kuanza kwa mchakato wa mabadiliko ya baadhi ya sheria ikiwa ni pamoja na kufufua mchakato wa Katiba mpya.

Habari Zifananazo

Back to top button