Lusajo, Mgunda watwaa tuzo Ligi Kuu

DAR ES SALAAM;MSHAMBULIAJI wa timu ya Mashujaa ya Kigoma, Reliants Lusajo ameteuliwa kuwa Mchezaji Bora wa mwezi Mei wa Ligi Kuu ya NBC msimu wa mwaka 2023/2024, huku Juma Mgunda wa Simba akichaguliwa Kocha Bora wa ligi hiyo kwa mwezi huo.

Taarifa iliyotolewa na Bodi ya Ligi Kuu nchini (TPLB), imesema Lusajo amewashinda Aziz Ki wa Yanga na Feisal Salum wa Azam alioingia nao fainali kwenye mchakato wa Tuzo za Mwezi uliofanywa na Kamati ya Tuzo za Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF).

“Kwa mwezi Mei, Lusajo alionesha kiwango kikubwa na kuwa msaada kwa timu yake katika ushindi wa michezo minne kati ya sita ambayo timu hiyo ilicheza, hivyo Mashujaa kukusanya pointi 12 na kupanda katika msimamo wa ligi kutoka nafasi ya 14 iliyokuwepo mwezi Aprili na kumaliza nafasi ya 8. Lusajo alifunga mabao matano na kuhusika katika mengine mawili.

“Mashujaa iliifunga KMC mabao 3-0, ikaifunga Tanzania Prisons mabao 2-1, Mtibwa Sugar mabao 3-2 na Dodoma Jiji mabao 3-0. Ilifungwa na Yanga bao 1-0 na pia ilifungwa na Tabora United pia bao 1-0.

“Kwa upande wa Mgunda aliongoza Simba kukusanya pointi 19 katika michezo saba iliyocheza, ikishinda sita na kutoka sare moja. Simba iliifunga Tabora United mabao 2-0, Azam mabao 3-0, Geita mabao 4-1, KMC bao 10, JKT Tanzania mabao 2-0 na ilitoka sare ya 1-1 na Kagera Sugar. Mgunda amewashinda Miguel Gamondi wa Yanga na Bruno Ferry wa Azam alioingia nao fainali,” imesema taarifa hiyo na kuongeza kuwa:

“Pia Kamati ya Tuzo imemchagua Meneja wa Uwanja wa Azam Complex, Chamazi Dar es Salaam, Amir Juma kuwa Meneja Bora wa Uwanja kwa  mwezi Mei kutokana na kufanya vizuri katika menejimenti ya matukio ya michezo pamoja na masuala yanayohusu miundombinu uwanjani.”

Habari Zifananazo

Back to top button