Lusinde ataka Dk Bashiru ajiuzulu

MBUNGE wa Mvumi, Livingston Lusinde (CCM) amemshauri Mbunge wa Kuteuliwa, Dk Bashiru Ali ajiuzulu ili Rais Samia Suluhu Hassan ateue mbunge mwingine.

Lusinde ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, alitoa ushauri huo jana Dodoma akishutumu kauli iliyotolewa na Dk Bashiru na kuilinganisha na uchochezi.

Hivi karibuni,  Dk Bashiru akiwa kwenye mkutano wa Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (MVIWATA) uliofanyika mkoani Morogoro alikaririwa na vyombo vya habari akionesha kukerwa na wanaoisifu serikali na wanaotumia neno la ‘anaupiga mwingi’

Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) juzi umemtaka Dk Bashiru aombe radhi kutokana na kauli yake ambayo walidai ina ukakasi.

“Nataka kumshauri Dk Bashiru kwa kuwa yeye anatokana na Ikulu, na anajisikia kichefuchefu Ikulu ikitajwa vizuri, kwa siasa za kiungwana Dk Bashiru anatakiwa kumpa mama nafasi ya kuchagua mbunge mwingine ambaye atamwelewa mama, mchezo anaoucheza na atakwenda naye sambamba,”alisema Lusinde.

Aliongeza “Huu ni uungwana, yeye ndiye aliyeimbisha mapambio ya kusifu, tulikokuwa tunasifu muimbishaji alikuwa ni Dk Bashiru anaimbisha mapambio ya kusifu, chama kilekile bado kinatawala, yule yule aliyekuwa Makamu wa Rais sasa hivi ndiye Rais anapata kichefuchefu gani sisi tunaposimama na kumsifu mama kwa mazuri anayofanya?”

Aliendelea, “Wakati Dk Bashiru akiwa Katibu Mkuu wa CCM na mshauri mkuu wa chama, bei ya kahawa ilikuwa kati ya shilingi 600 hadi shilingi 700 kwa kilo, sasa yeye si katibu mkuu bei ya kahawa imekuwa shilingi 2,000. Hapa hataki tusema mama ameupiga mwingi…”

Aliongeza, “tumshukuru Rais, juzi alikuwa China, tumeona namna alivyopata soko kubwa la kuuza parachichi, kabla ya hapo tulikuwa hatupeleki hata parachichi moja kwa sasa wakulima wanaweza kupeleka parachichi zao, Dk Bashiru hataki tumpongeze Rais kwamba amefanya kazi”.

Lusinde alisema wakati wote Dk Bashiru alipokuwa kiongozi mkuu wa CCM, bajeti ya Wizara ya Kilimo ilikuwa Sh bilioni 250 na tangu Rais Samia alipoingia madarakani, imeongezeka hadi kufikia Sh bilioni 950.

“Serikali haina dini lakini wananchi wake tuna dini. Hata kwenye dini tunatakiwa kushukuru Mungu tukipata au tusipopata tunatakiwa kushukuru Mungu.

Sasa kwa nini tusimshukuru Rais kwa kazi kubwa anayoifanya.”

Habari Zifananazo

Back to top button