Ma- RPC wafanyia kazi maagizo ya Samia

MAKAMANDA wa polisi wa mikoa wameanza kufanyia kazi maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa hivi karibuni kuhusu maadili ya polisi.

Rais Samia alitoa maagizo hayo wakati akizungumza na viongozi wakuu wa Jeshi la Polisi Moshi mkoani Kilimanjaro.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Henry Mwaibambe ofisa wa polisi mkoani humo atakayelichafua jeshi hilo atashughulikiwa.

Kamanda Mwaibambe alisema polisi yeyote ndani ya mkoa wa Geita anapaswa kuzingatia kiapo cha utumishi, maadili na uwajibikaji badala ya kutanguliza maslahi binafsi.

“Mimi kama Kamanda wa Mkoa nitawangalia wote waliopo chini yangu na wao wakiwa wananiangalia mimi, kwa hiyo ni suala la utumishi msawazo, mimi nitasimamia waliopo chini yangu na wao watasimamia wa chini yao. Taratibu zipo wazi, ukikengeuka adhabu yake ni hii, na adhabu ipo kwa kila kosa, hakuna kosa ambalo halina adhabu, ukiendekeza ulevi, kutoenda kazini, adhabu ipo wazi” alisema.

Kamanda Mwaibambe alisema alichokisema Rais Samia kuhusu maadili ni cha kweli hivyo kajipanga na atachukua hatua.

“Makamanda wote tumeazimia kutekeleza yale maagizo yote aliyotuambia. Sisi tuna sheria zetu kwa hiyo kama kuna mtu anafanya yale ambayo hayaendani na taratibu zetu tutamchukulia hatua bila kumuonea haya”alisema.

Kamanda Mwaibambe aliahidi kufuatilia kwa ukaribu tuhuma za matumizi mabaya ya mafuta na kaonya yeyote mwenye tabia hiyo ajiandae.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ulrich Matei alisema atatembelea wilaya zote aonane na askari awape maelekezo kuhusu maadili.

Kamanda Matei alisema watawakumbusha askari maadili ili wafanye kazi kwa kuzingatia miongozo ya kazi.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Kigoma, Filemon Makungu alisema miongoni mwa hatua wanazochukua ni kuhakikisha mwongozo wa utendaji wa jeshi la polisi (PGO) unazingatiwa.

Kamanda Makungu alisema baadhi ya watendaji wa polisi wanatuhumiwa kwa rushwa kwa askari wa uplelezi na wa usalama barabarani hivyo watachunguza na kuhuchukua hatua.

Aidha alisema watahakikisha uchunguzi unazingatia miiko, maadili na bila kukomoa au kumuumiza mtu kwa kukusudia.

Kamanda Makungu alisema wataendelea kutoa maelekezo kwa watendaji wasitumie nguvu kubwa wakati wa ukamataji ili kuondoa malalamiko ya uonevu.

Alisema jamii inapaswa kutii sheria bila shuruti na akasema polisi jamii itatumika kwa kiasi kikubwa kutekeleza maagizo ya Rais Samia.

Pamoja na maagizo ya Rais Samia, hivi karibuni Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango alimuagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi, Camillus Wambura ashughulikie malalamiko ya wananchi kwa Jeshi la Polisi na kuwachukulia hatua askari wachache wanaoharibu taswira ya jeshi hilo.

Dk Mpango alitoa maagizo hayoofisini kwake Dar es Salaam alipokutana na kuzungumza na IJP Wambura.

Aliliagiza Jeshi la Polisi litende haki bila kuonea mtu na yeyote anayevunja sheria achukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria na si vinginevyo.

Dk Mpango alilipongeza jeshi hilo kwa kuendelea kuimarisha amani na ulinzi wa wananchi na mali zao.

Alisema kazi ya kulinda raia na mali zao ni msingi wa maendeleo ya nchi hivyo Jeshi la Polisi linapaswa kuhakikisha kunakuwa na utulivu wakati wote.

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button