Maabara ya MSA kivutio upimaji madini
GEITA; ZAIDI ya sh bilioni 5 za Kitanzania zimewekezwa katika maabara ya MSA inayopima sampuli za madini kwa kiwango cha kimataifa mkoani Geita.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Maabara ya MSA, Mugisha Lwekoramu, wakati wa ufunguzi wa maabara hiyo iliyoanzishwa mwaka 2020 ikiwa ni kampuni tanzu ya MSALABS yenye makao makuu yake nchini Canada.
Akizungumzia kuhusu teknolojia inayotumika katika maabara hiyo Lwekoramu amesema maabara hii inatumia teknolojia ya kisasa ya upimaji wa sampuli kwa mionzi (PhotoAssay), ambayo ni rafiki kwa utunzaji mazingira kwa sababu haitumii kemikali au moto katika upimaji sampuli.
Akielezea kuhusu ufanisi wa teknolojia hiyo, amesema ni sehemu ya mapinduzi ya teknolojia kwa sababu inamuwezesha mdau kupata majibu ya sampuli ndani ya saa mbili ukilinganisha na teknolojia ya zamani ya kutumia moto na kemikali.
Kwa upande Waziri wa Madini Anthony Mavunde amempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa maabara hiyo kwa kufanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya madini , akiwataka kuendelea kufungua matawi mengine nchini.
Mavunde ameahidi kuwa Serikali Awamu ya Sita itaendelea kuwatengenezea mazingira rafiki ya uwekezaji na kutoa ushirikiano kwa jinsi itakavyohitajika katika mnyororo mzima wa sekta ya madini.