Maafisa tarafa, watendaji wa kata watakiwa kutenda haki

BARIADI: Serikali imewataka maafisa tarafa na watendaji wa kata katika Mkoa wa Simiyu kufuata misingi ya haki katika utekelezaji wa majukumu yao hasa wakati wa kuwahudumia wananchi.

Mbali na hilo wametakiwa kuhakikisha wanasimamia masuala ya ulinzi na usalama katika maeneo yao ya kazi, na wasiwe visababishi kwa wananchi kukosa imani na serikali katika masuala ya ulinzi na usalama.

Maagizo hayo yametolewa na Mkuu wa Wilaya ya Itilima mkoani humo, Anna Gidalya alipomwakilisha Mkuu wa Mkoa huo Dk Yahaya Nawanda kufunga mafunzo ya siku mbili ya watumishi hao yaliyotolewa na Ofisi ya Rais –TAMISEMI.
Gidalya amesema kuwa wananchi wamekuwa na kero nyingi kwenye maeneo yao, ambapo aliwataka maafisa tarafa na watendaji wa kata hao, kuhakikisha wanasikiliza kero hizo na wanazitatua kwa haki.

“Moja ya jukumu lenu kubwa ni kusikiliza kero za wananchi na kuzipatia ufumbuzi, niwatake mnapomaliza mafunzo haya, nendeni kusikiliza kero za wananchi na mzitatue kwa haki, mtendaji wa kata hupaswi kulalamikiwa na mwananchi kuwa haujatenda haki,” amesema Gidalya.

Aidha Mkuu huyo wa Wilaya aliwataka watendaji hao, kuhakikisha suala la ulinzi na usalama linakuwa jukumu lao la kwanza, kwa kuwashirikisha wananchi na vyombo vya ulinzi na usalama vilivyopo kwenye maeneo yao ili kuwepo na amani.

Habari Zifananazo

Back to top button