DAR ES SALAAM: RAIS Samia Suluhu Hassan ametoa maelekezo matano kwa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari pamoja na Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (TDPC) ili kudhibiti uvujaji wa taarifa binafsi za mtu au taasisi na anataka kuona matokeo ndani ya mwaka mmoja.
Akizungumza leo Aprili 3, 2024 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam, Rais Samia ameagiza Tume ya Ulinzi ya Taarifa Binafsi ihakikishe taasisi zote za umma na binafsi zinasajiliwa na kutekeleza taarifa ya ulinzi binafsi kabla ya Desemba mwaka huu.
Pili, ameelekeza Taasisi zinazokusanya na kuchakata taarifa binafsi, zihakikishe zinazingatia matakwa ya sheria ya ulinzi wa taarifa binafsi, na ameitaka tume kutoa elimu, kusisitiza wajibu wa taasisi hizo.
Aidha, Rais Samia amemuelekeza Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kuhakikisha wanatekeleza vema sera na kufuatilia kwa karibu kazi za tume.
Pia, ameitaka Ofisi ya Waziri Mkuu isimamie na kuhakikisha mifumo ya TEHAMA yote inasomana mpaka ifikapo Desemba.
Aidha, Rais Samia amesema kuna taasisi muhimu ambazo zipo maeneo mbali mbali mfano NIDA ipo Wizara ya Mambo ya Ndani, IGA ipo Utumishi, na tume hi ya taarifa binafsi ipo ndani ya wizara ya habari hivyo kuwe na mratibu ambaye yupo ‘Neutral’ kwamba taasisi zote ambazo zipo maeneo mbalimbali zinakuwa ‘regulated’ vizuri, na pengine ziangaliwe sheria inayounda taasisi hizo ili kusaidiana.