Maagizo yatolewa kwa wadau huduma za wanyama

DAR ES SALAAM: WAZALISHAJI na Wasambazaji wa rasilimali na vyakula vya wanyama wametakiwa kuhakikisha vyakula na viwanda vyao vimekaguliwa ili kufikia ubora na usalama unaohitajika.

Mkurugenzi wa Huduma za Uchunguzi kutoka Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), iliyoko chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk Zacharia Makondo amesema hayo wakati wa kuhitimishwa kwa ziara ya kikazi ya siku tatu ya wakaguzi wa vyakula vya Mifugo.

Amesema wakaguzi hao wamekagua baadhi ya viwanda, wauzaji wa vyakula vya mifugo na kuwatembelea baadhi ya wafugaji wanaotumia vyakula hivyo.

Dk Makondo amesema ni muhimu kwa vyakula vya mifugo kufika sokoni kama vilivyowekwa viwandani, na kuonya wanaopuuzia kupima na kuhuisha usajili wa viwanda vyao kwa kueleza kuwa watachukuliwa hatua za kisheria.

Amesema wale ambao hawajasajiliwa watafungiwa, hawataruhusiwa kufanya shughuli hiyo.

Kwa upande mwingine amesema maabara za kanda zitawezeshwa kuwa na vifaa vya kufanya ukaguzi katika maeneo ambayo yanauhitaji mkubwa wa kufanywa kwa ukaguzi wa rasilimali za vyakula na vyakula vya mifugo ili kuhakikisha vinakuwa salama.

Kwa upande wake Mtaalamu wa Mifugo, Idara ya Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Theodata Sallema, amewakumbusha wakaguzi kufanya ukaguzi katika maeneo yao ili kuhakikisha wadau wanafuata sheria.

Naye Meneja wa TVLA Kanda ya Kaskazini – Kituo cha Arusha, Dk Rowenya Mushi amesema kanda hiyo imepata chachu ya kuongeza nguvu katika kutoa elimu kwa wazalishaji na wasambazaji wa vyakula vya mifugo juu ya kupima vyakula vyao kuwa na ubora na kuleta matunda kwa wafugaji.

“Chakula bora huwa kinaleta mazao bora kwa wafugaji na hilo ndio lengo kuu la Wizara ya Mifugo na Uvuvi na serikali kwa ujumla, kuhakikisha mfugaji anafuga kisasa na kupata chakula bora kwa ajili ya mifugo yao hatimaye kupata mazao bora na kupata kipato kizuri zaidi na kukuza uchumi,” amesema.

TVLA inatarajia kuendelea kutoka elimu na kufanya ukaguzi wa rasilimali na vyakula vya mifugo katika kanda mbalimbali za wakala hiyo pamoja na kusimamia sheria ili wafugaji ili waweze kufuga kwa tija na kupata matokeo bora kupitia ufugaji.

Habari Zifananazo

Back to top button