Maambuzi VVU yapungua 4%

KASI ya maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi imepungua kutoka asilimia 7 mwaka 2003 hadi kufikia asilimia 4.3 mwaka 2022.

Hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk Grace Magembe, akimuwakilisha Waziri wa Afya,Ummy Mwalimu wakati akiongoza ujumbe wa wageni kutoka Mfuko wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Ukimwi.

Dk Magembe amesema kupitia ufadhili wa Pepfar Tanzania imeweza kuanzisha vituo tisa vya utoaji wa dawa ya Methadone kwa waathirika wa dawa za kulevya nchi nzima, pamoja na huduma ya kliniki ya kutembea katika vituo saba.

Advertisement

“Tanzania imepiga hatua kubwa katika kuimarisha huduma za afya, hasa katika huduma jumuishi kwa waathirika wa dawa za kulevya na VVU.” amesema Dk Magembe.

Ameishukuru Serikali ya Marekani kwa msaada wake kupitia Mfuko wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Ukimwi (PEPFAR) kwa kuendelea kushirikiana katika uboreshaji wa huduma za afya nchini na mapambano dhidi ya Virusi vya Ukimwi.

Kwa upande wake,Kaimu Naibu Mratibu Mkuu wa masuala ya Ukimwi wa Mfuko wa Dharura wa Rais wa Marekani wa UKIMWI (PEPFAR), Dk Rebecca Bunnell ameishukuru Serikali ya Tanzania kumkaribisha kuja kuona shughuli za PEPFAR Mkoani Tanga na pia alishukuru kwa ushirikiano unaonyeshwa na Serikali ya Tanzania katika mapambano ya VVU na UKIMWI nchini.

Dk Rebecca amepongeza juhudi zinazofanywa na serikali kuimarisha huduma za afya nchini na kuahidi kuwa Serikali ya Marekani itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuboresha zaidi huduma za afya.

Ujumbe huo ulitembelea Mkoa wa Tanga katika Ofisi za Mkuu wa Mkoa,Waziri Kindamba pamoja na Kituo cha Warahibu wa Dawa za Kulevya “Gift of Hope” kilichopo Jijini Tanga.

1 comments

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *