MKUU wa Mkoa wa Morogoro , Adam Malima amewataka washiriki wa maonesho ya wakulima na wafugaji maarufu Nanenane ya Kanda ya Mashariki yanayofanyika viwanja vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kukamilisha maadalizi yao kabla ya Julai 29 mwaka huu.
Ametoa agizo hilo wakati alipotembelea mabanda na vipando kabla kuzinduliwa kwa maonesho hayo Agosti mosi mwaka huu ambayo yanashirikisha mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Tanga na Morogoro inayounda Kanda ya Mashariki.
RC Malima alifurahishwa kuona baaadhi ya halmashauri zinazoshiriki maonesho hayo zikiwemo Manispaa ya Morogoro na Kigamboni na nyingine kuonekana zimejiandaa vizuri .
” Tarehe 29,2023 tunatarajia kila halmashauri na waoneshaji wengine wawewameshafanya mambo yao yakiwa yamekamilika Ili tarehe 30 tuanze maonesho.” alisema Malima
Malima alisema Kanda ya Mashariki imekuwa mara zote inafanya vizuri katika maonesho ya Nanenane hivyo amewataka wadau wote wa Kanda hiyo kuendeleza sifa hiyo ya kufanya vizuri.
Kwa upande wake, Katibu Tawala Msaidizi sehemu ya Uchumi na Uzalishaji Mali wa mkoa huo, Dk Rozalia Rwegasira alisema zaidi ya Taasisi 500 watashiriki katika Maonesho ya mwaka huu (2023) ambayo ni sawa na asilimia 100 ukilinganisha na maonesho ya mwaka jana (2022) ambapo wadau na Taasisi 400 pekee walishiriki.
Dk Rozalia alisema kuwa katika maonesho ya mwaka huu wakulima watajifunza teknolojia ya malisho ya mifugo kwa lengo la kukabiliana na changamoto ya wafugaji kukosa malisho ya mifugo wao.
Alisema Wakulima nao watapata elimu bora ya kilimo cha viungo imiwemo Karafuu, Pilipili Manga na mdarasini.
Maonesho ya Nane nane 2023 ni maonesho ya 30 tangu kuanzishwa kwake na kauli mbiu ikiwa ni ”Vijana na Wanawake ni msingi imara wa mifumo endelevu ya chakula”.
Maandalizi hayo yameshika kasi baada ya agizo la mkuu wa mkoa huyo ambapo waoneshaji wakiwa katika pilika pilika kukamilisha mabanda yao likiwemo Banda la Halmashauri ya wilaya ya Chalinze.
Comments are closed.