WAZIRI wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Zanzibar, Shamata Shaame, amesema maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani itakayoadhishwa Kisiwani Pemba, Oktoba 10 hadi 16 yamekamilika kwa asilimia 70.
Shaame amesema hayo alipokuwa akizungumza na HabariLeo, kuhusu maandalizi hayo, ambayo yatagharimu sh bilioni 1.2, fedha ambazo zinatolewa na wadau mbalimbali wa kilimo pamoja na benki, ili kuweza kutengeneza miundombinu ya maji, umeme, mahema, uzio pamoja na njia za kupita.
Amesema hadi kufikia jana taasisi za kifedha karibia zote kisiwani humu pamoja na wadau wa kilimo, wameonesha nia ya kutoa michango yao, ili kuhakikisha maadhimisho hayo yanafanikiwa.
“Maeneo yote tupo vizuri isipokuwa kwenye fedha bado tuna uhitaji. Vipando vya mazao mbalimbali vilivyopandwa vimeota, hatua iliyofikiwa sasa ni ya kuweka mabanda,” amesema.
Amesema mpaka sasa taasisi 165 zimeonesha nia ya kushiriki katika maadhimisho hayo.