Maandalizi ya Michezo ya Afrika 2023 ianze mapema

MICHEZO ya 13 ya Mataifa ya Afrika itafanyika Accra, Ghana mwakani na Tanzania ni miongoni mwa nchi 53 zinazotarajia kushiriki michezo hiyo.

Wachezaji watakaoshiriki watatumia michezo hiyo kama maandalizi kwa ajili ya kufuzu kushiriki Michezo ya Olimpiki itakayofanyika Paris, Ufaransa mwaka 2024.

Michezo ya 22 ya Jumuiya ya Madola ndio kwanza imemalizika na Tanzania tumerudi na medali tatu, moja ya fedha na mbili za shaba ni jambo la kujivunia, kwani kwa takribani miaka 16 hatukuwahi kurudi na medali katika michezo hiyo.

Advertisement

Imebaki chini ya mwaka mmoja kabla ya kufanyika kwa michezo hiyo ya Afrika, hivyo mashirikisho na vyama vya michezo vianze maandalizi mapema kwa ajili ya kupeleka timu.

Michezo hiyo kama ile ya Olimpiki na Jumuiya ya Madola, nayo uratibiwa na Kamati za Olimpiki za nchi (NOC), hivyo ni jukumu la vyama au mashirikisho ya michezo, serikali kuungana na TOC kuanza maandalizi mapema.

Hakuna siri kwani siku zote maandalizi ya mapema imekuwa yenye manufaa, kwani tumeona maandalizi ya timu zetu kushiriki michezo iliyopita ya Jumuiya ya Madola imeleta tija na kutuwezesha kurudi na medali tatu.

Huwezi kuiweka kando serikali kwa mafanikio yaliyopatikana katika Michezo ya Jumuiya ya Madola ya mwaka huu, kwani yenyewe chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ilitoa fedha na kuzifanya timu kukaa kambini kwa muda mrefu.

Ni jambo la aina yake kuona timu zetu tangu Februari ziko kambini kwa ajili ya michezo iliyokuja kufanyika kuanzia Julai hadi Agosti.

Kwa miaka mingi wachezaji na mashirikisho ya michezo au na vyama vya michezo wamekuwa wakiililia serikali kutaka isaidie timu kukaa kambini mapema, kilio ambacho imekisikia.

Ni matarajio ya safu hii kuwa mashirikisho ya michezo kwa kushirikiana na serikali kupitia Wizara husika na michezo na Baraza la Michezo la Taifa (BMT) wataanza kukutana mapema kwa ajili ya maandalizi ya michezo hiyo ya Afrika.

Kwa mara ya mwisho Tanzania ilitwaa medali katika Michezo ya Jumuiya ya Madola ilikuwa miaka 16 iliyopita wakati Samson Ramadhani na Fabian Joseph walipotwaa medali ya dhahabu na fedha katika marathoni na mbio za meta 10,000.

Na katika mchezo wa ndondi, ambao mwaka huu umetupatia medali mbili za shaba, wenyewe kwa mara ya mwisho ulituletea medali miaka 24 iliyopita wakati bondia Michael Yombayomba (sasa marehemu) alipotwaa dhahabu katika Michezo ya Kuala Lumpur, Malaysia mwaka 1998.

Ni miaka mingi imepita, hivyo ushindi huu wa mwaka huu unatakiwa kuwa na mwendelezo kama ilivyokuwa huko nyuma wakati Tanzania iking’ara katika michezo mbalimbali ya kimataifa na hasa katika riadha na ngumi.

Ushindi ni gharama na hauji kama mvua, hivyo wakati umefika wa kutumia fedha kwa ajili ya kuziandaa timu zetu ili zifanye vizuri katika mashindano mbalimbali ya kimataifa.