Maaskofu kumpokea Kardinali Rugambwa leo

MWADHAMA Protase Kardinali Rugambwa (63) anatarajiwa kurejea nchini leo akitoka Vatican alikosimikwa kuwa kardinali.

Septemba 30, mwaka huu Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis alisimika maaskofu 21 kuwa makardinali akiwamo Rugambwa.

Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Dk Charles Kitima, amesema Kardinali Rugambwa anatarajiwa kuwasili saa saba mchana kwa ndege ya Shirika la Ndege la Ethiopia na akitoka hapo atapelekwa TEC kwa ajili ya hafla ya kumpongeza.

“Viongozi mbalimbali wa Kanisa Katoliki watakuwepo hapa kumpongeza kwa ujumbe mbalimbali lakini pia tunatarajia kuwa na viongozi wa serikali,” alisema Dk Kitima.

Alisema wanatarajia Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba kushiriki hafla hiyo.

Julai 9, mwaka huu, Papa Francis alimteua Askofu Mkuu Rugambwa kuwa Kardinali na anakuwa Mtanzania wa tatu kupata nafasi hiyo akitanguliwa na Mwadhama Laurean Kardinali Rugambwa na Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo.

Kabla ya hapo alikuwa Askofu Mwandamizi wa Jimbo Kuu la Tabora tangu Aprili mwaka huu. Alizaliwa Mei 31, 1960, Bunena mkoani Kagera. Septemba 2, 1990, Papa Yohane Paulo II alimpa daraja la upadri katika viwanja vya Jangwani, Dar es Salaam.

Mwaka 1994 hadi 1998 alikwenda Roma kwa masomo ya Shahada ya Uzamivu katika theolojia ya uchungaji kisha alirudi Tanzania.

Mwaka 2002 aliitwa Roma kufanya kazi katika ofisi ya Idara ya Uinjilishaji wa Mataifa kazi aliyoifanya kwa miaka sita.

Januari mwaka 2008, Papa Benedikto XVI alimteua kuwa Askofu wa Jimbo la Kigoma. Mwaka 2012 aliitwa tena kufanya kazi katika makao makuu ya Kanisa Katoliki, Roma hadi Aprili mwaka huu alipoteuliwa kuongoza Jimbo Kuu la Tabora.

Habari Zifananazo

Back to top button