Maaskofu wakemea mahubiri ya uongo

MAASKOFU wa Kanisa la Anglikan Tanzania wamekemea chimbuko la makanisa yanayoeneza mahubiri ya uongo na kujinufaisha kupitia ongezeko la watanzania wanaodanganyika kupata mali bila kufanya kazi na changamoto zao zingine kushughulikiwa kwa haraka.

Pamoja na mahubiri ya uongo, maaskofu hao wamezungumzia mmomonyoko wa maadili na anguko la mila na desturi za watanzania wakisema mambo hayo yakiachwa yaendelee taifa litaangamia.

Advertisement

Wameyasema hayo leo kwenye kongamano lao la kitaifa la uinjilisti linalofanyika katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Mkwawa, mjini Iringa ikiwa ni mara ya kwanza katika historia ya kanisa hilo nchini.

Askofu wa Anglikan Dayosisi ya Ruaha (Iringa), Dk Joseph Mgomi alisema kanisa limewaita katika kongamano hilo wainjilisti hao kutoka nchi nzima ili wakae pamoja, kushauriana, kubadilishana uzoefu na maarifa yatakayowaweza kubadili mbinu itakayosaidia kufikisha injili ya kweli kwa wananchi.

“Injili ni ile ile iliyoandikwa karne ya kwanza na mpaka leo haijabadilika-lakini jamii tunayoihudumia inabadilika kila siku na sehemu yake imeanza kujitenga na imani ya kweli kwasababu kuna sauti nyingi zimeibuka zinazofundisha mahubiri ya uongo na kishetani,” alisema Askofu Dk Mgomi.

Alisema wanaofanya kazi hiyo ya kueneza mahubiri hayo wanafanikiwa kama alivyofanikiwa shetani kwasababu wanachanganya uongo na ukweli kidogo na hivyo kuziteka roho za watanzania wengi hususani wanawake.

Naye Askofu Julius Lugendo wa Kanisa Anglikana Dayosisi ya Southern Highlands (Mbeya), alisema kongamano hilo litasaidia kuleta umoja wa kanisa na uamsho kwa wainjilisti kufanya kazi ya kueneza injili ya kweli na kwa haraka ili kuinusuru jamii isiendelee kuhangamia.

“Tunaishi katika nyakati ngumu zilizojaa uharibufu wa kila namna na maadili yamepotea, hivyo ni muhimu tukawawezesha wainjilisti wetu wakaeneze injili katika nyakati hizi zilizobadilika ili tuwe na taifa lenye amani, staha na kumcha mungu kwa njia za kweli,” alisema.

Askofu Lugendo alisema dunia na Tanzania ya sasa imejaa mafundisho mengi yasio ya kweli na binadamu wanayakimbilia mafundisho hayo kwasababu yanawapa matumaini ya uongo yaliyojaa Imani ya kujipatia vitu au mali bila kufanya kazi na kuponya matatizo yao mengine.

“Kuna wahubiri wanaowaambia waumini wao wafungue pochi na baada ya muda fulani fedha zitajaa bila kufanya kazi yoyote. Uongo kama huu umeendelea kuaminiwa na wananchi wengi na tunaona jinsi Taifa linavyoelekea kuhangamia, hivyo ni lazima sisi kama kanisa tuchukue hatua,” alisema.

Alisema baada ya kongamano hilo, wainjilisti hao watashuka katika ngazi ya jamii na kuielimisha namna ya kujiondoa na mafundisho ya uongo, kufanya kazi na kumcha Mungu ili kuleta matokeo chanya kwa Taifa.

“Kwa kupitia kongamano hili tutajitahidi pia  kuelimisha watu wetu umuhimu wa kutunza mila na desturi zetu nzuri katika kupambana na uharibifu unaoosababisha ukatili wa kijinsia, kushamiri kwa vitendo vya usagaji na ushogan na baadhi ya watanzania kukataa kutambua jinsi zao hatua inayowafanya wanaume wanaishi kama wanawake na wanawake kama wanaume,” alisema.

Kwa upande wake Askofu Johnson Chinyong’ole wa Dayosisi ya Shinyanga alisema mpango wa kanisa hilo kueneza injili ya kweli kwa watanzania inatekelezwa kupitia mkakati wao unaolenga kuifikia kila kata ifikapo mwaka 2027.

“Katika maeneo mengi wapo watu wengi bado hawajamjua Mungu wa kweli na ndio maana wanahangukia katika mahubiri ya uongo. Kwa utafiti wetu tutahitaji kufika pia katika shule zote, vyuo vya kati na vyuo vikuu,” alisema.

Askofu Chinyong’ole alisema mpango huo wa kueneza injili kwa watu wote utawafikia pia wasomi wa fani mbalimbali nchini kote ambao ni waumini wa dhehebu hilo.

“Kutokana na kasi ya kuenea kwa mahubiri ya uongo tunatengeza watu watakaosimama na kuliombea Taifa ili lisiendelee kuhangamizwa na mahubiri ya uongo,” alisema.

3 comments

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *