MAGONJWA yasiyoambukiza ni ambayo vimelea vyake haviwezi kusambazwa kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine.
Mfano wa magonjwa hayo ni ya moyo na mishipa ya damu, saratani, ya mfumo wa hewa, kisukari, magonjwa ya akili na ajali.
Magonjwa hayo yanaongezeka kwa kasi na kuwaathiri hata watu wenye umri mdogo wakiwemo watoto.
Kwa mwaka 2016 vifo milioni 42 sawa na asilimia 71 vilivyoripotiwa duniani vilitokana na magonjwa hayo. Asilimia 75 ya vifo vyote vilivyohusisha watu wenye miaka 30 hadi 70 husababishwa na magonjwa hayo.
Kwa Tanzania inakadiriwa kuwa magonjwa yasiyoambukiza yanasababisha asilimia 27 ya vifo vyote. Tafiti za mwaka 2012 zilionesha kuwa kwa kila watu 100 wenye miaka 25 na kuendelea, tisa wana kisukari, 26 wana shinikizo la damu, 25 wana mafuta yaliyozidi kwenye damu na 34 wana uzito uliopitiliza.
Aidha, tafiti za miaka ya 1986/1987 zilionesha kuwa ni mtu mmoja tu kwa kila watu 100 alikuwa na kisukari na watu watano kwa kila 100 walikuwa na shinikizo la damu. Sababu za kuongezeka kwa magonjwa hayo kwa kiasi kikubwa ni mtindo wa maisha ikijumuisha ulaji mbaya na kutokufanya mazoezi.
MABADILIKO TABI ANCHI YATAJWA
Licha ya sababu hizo wataalamu pia wameeleza kuwa mabadiliko ya tabia nchi yamekuwa yakichangia ongezeko la magonjwa ya moyo na saratani. Wataalamu hao wanasema ongezeko la joto, ukame na uchafuzi wa hewa na mazingira pia yanachangia ongezeko la magonjwa sugu ya mfumo wa hewa.
Wakizungumza na HabariLEO katika mahojiano, kwa nyakati tofauti wataalamu hao wanasema kadiri mazingira yanavyobadilika mwili unabadilika kutoka katika mifumo iliyozoea na kwenda katika mifumo mingine migeni.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Dk Peter Kisenge anaeleza kuwa kunapokuwa na ukame watu hawapati lishe bora hivyo wanawake wanaopata ujauzito hawapati lishe inayohitajika kama madini ya aina mbalimbali kama folic ambayo yanapatikana katika mbogamboga na matunda hivyo watoto wanaweza kuzaliwa wakiwa na matatizo ya moyo kama matundu.
“Lakini pia kutokupata hewa safi inaweza kuchangia magonjwa ya moyo, mapafu ambayo inaleta magonjwa ya pumu, viwanda kuongezeka vinavyotoa kemikali vinaweza kuleta madhara,” anafafanua Dk Kisenge.
Anasema wagonjwa wa shinikizo la damu wanapopata joto kali wanapata msongo wa mawazo hali inayofanya moyo kwenda mbio, kuchoka na wanaweza kupata kiharusi. “Mabadiliko ya tabianchi yanaweza kuletwa na binadamu na wanyama shughuli za ujenzi wa viwanda, kukata miti na mengine ni visababishi,” anasema Dk Kisenge.
Anawashauri wananchi kupenda kupima afya kwani wanapopima wanaweza kugundulika mapema, wazingatie lishe bora, kufanya mazoezi mara tatu kwa wiki kwa muda wa nusu saa.
“Waepuke uvutaji wa sigara, unywaji wa pombe uliokithiri ni hatari yakiepukwa wanaweza kuepusha magonjwa ya moyo na ni magonjwa yanayoleta madhara makubwa na ni gharama kubwa pia,” anasisitiza.
KUBADILIKA KWA TABIA YA MWILI Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Kisukari, Profesa Andrew Swai anabainisha kuwa magonjwa kama kisukari, saratani, presha yanatokana na jinsi mwili unavyojishughulisha na vitu ambavyo si vya kawaida.
“Mtu anaweza kuwa na pumu kwa sababu kuna vitu ambavyo akigusa kama manyoya ya paka mwili wake unaona hiki ni hatari unapambana, namna gani mwili wako unapambana na vitu ambavyo si vya asili yako na jinsi ulivyopambana na vitu hivyo akiwa mdogo.
“Kama leo umejifungua kwa njia ya kawaida yule mtoto anapopita kwenye njia ya uzazi anabeba vijidudu vyote vilivyomo na miili inazoea na akijifungua kwa njia ya upasuaji vile vijidudu havipo tena kwa sababu anatolewa na kufungwa na nguo hagusi vijidudu sasa mwili wake haujui kama hao ni marafiki unaanza kupambana nazo,” anasema.
Profesa Swai anasema kwa sababu ya mabadiliko ya tabianchi na mazingira yanabadilika, mfumo wa maisha unabadilika na aina ya vyakula pia vinabadilika.
UKAME UNAVYOKUWA SABABU Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Profesa Fransis Furia anabainisha kuwa kukiwa na ukame majani hayaoti na wanyama hawakai na kwa kawaida muunganiko wa wanyama na watu vinasaidia kupunguza baadhi ya magonjwa.
Anasema zamani ilikuwa inaaminika magonjwa kama pumu na mzio yalikuwa hayatokei vijijini kwa sababu wanacheza kwenye matope, wanakutana na minyoo na wadudu kwenye udogo.
“Kwa hiyo wanapokuwa kule na ule uhusiano waliokuwa nao na watoto wananyonya maziwa ya mama, kunyonya maziwa ya mama na kucheza katika mazingira hayo ya udongo na wanyama kunawasaidia kutopata pumu na msio. “Sasa hivi kwa sababu ya mabadiliko mvua hazinyeshi na wadudu wanakufa kwa hiyo hatukutani nao, sasa hivi tunajenga nyumba tunaweka ‘tails’ (vigae) hawataki watoto kupata udongo tunataka wacheze huko wakutane na wadudu na wawazoee,” anaeleza Profesa Furia.
Anasema uchafuzi wa hali ya hewa unachangiwa pia na moshi kama wa sigara ambao una madhara makubwa kwa watu ambao wako karibu na watumiaji. Profesa Furia anaeleza kuwa jua kali pia linawaathiri watu wenye ulemavu wa ngozi kwani jua kali husababisha kupata saratani.
“Ni lazima tuhusishe jamii nzima kuhusu magonjwa haya ili kila mtu ajikinge na magonjwa haya,” anasisitiza Profesa Furia.
MADHARA YA JOTO KALI
Naye mtaalamu wa mabadiliko ya tabianchi na mazingira, Richard Mayungi anasema ni kweli mabadiliko ya tabianchi yanaweza kuchangia magonjwa yasiyoambukiza kwa kubadili mfumo wa maisha ya binadamu mfano joto kuongeza mapigo ya moyo. Aidha, anaeleza kuwa kama mwili wa binadamu umezoea nyuzi joto 24 halafu hali ikabadilika kuwa nyuzi joto 28, lazima mfumo utahitaji maji mengi na upumuaji unabadilika.
“Ikitokea sasa hali ya hewa imekuwa ya joto mapigo ya moyo yanakwenda mbio, wenye viashiria vya shinikizo la damu linaongezeka na ikitokea kuna mabadiliko makubwa kwenye mazingira kwa kiasi kikubwa mifumo ya mwanadamu mfano aina ya vyakula ikibadilika basi aina ya vyakula vinaweza kubadilisha mwili na kuleta magonjwa yasiyoambukiza,” anafafanua.
Pia anasema hewa inaweza kubadilisha mfumo wa binadamu na kuleta magonjwa ya ziada ambayo hayaambukizi. Naye Mkurugenzi wa Shirika la AMREF Tanzania, Dk Florenc Temu anaeleza kuwa mabadiliko ya hali ya hewa yanaleta mambo mengi kama kuongezeka kwa joto, ukame, uhaba wa chakula, mwili kuchoka na mengine.
Anaongeza: “Tunafahamu kuwa jua linatoa mionzi na wenzetu albino wanasumbuliwa na saratani ya ngozi hivyo jua linapokuwa kali wanaathirika zaidi na saratani za ngozi.”