Mabadiliko tabianchi, mbegu za alizeti kufanyiwa utafiti

ILI kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi ikiwemo ukosefu wa mvua Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI) Ilonga iliyopo Wilaya ya Kilosa Mkoani Morogoro imeanza kufanya tafiti kwa aina 50 ya mbegu za alizeti.

TARI inafanya utafiti kwa kushirikiana na Taasisi ya Kuboresha Mifumo ya Masoko ya Kilimo Tanzania (AMDT)ambayo imewekeza zaidi ya Sh Bilioni nne kuwezesha miradi ya kuendeleza sekta za mazao ya Alizeti na mikunde nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati walipotembelea kituo cha TARI Ilonga iliyopo Kilosa, Morogoro, Mtaifiti Msaidizi wa Idara ya Alizeti,Beatrice Nnko amesema wanafanya jaribio la vinasaba vya alizeti ambazo zimekusanywa kutoka maeneo mbalimbali ndani na nje ya Tanzania.

Nnko amebainisha kuwa Lengo la jaribio hilo ni kugundua tabia za alizeti ambazo zinaweza kusaidia katika kuzalisha mbegu ambazo zitaweza kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi ambapo kwasasa hali ya hewa imekuwa ikibadilika.

Amefafanua kuwa wanafanya utafiti ili kuweza kuendana na mabadiliko ya tabia ya nchi kwa sehemu tofautitofauti na kila mbegu inatabia yake ambapo nyingine zinaweza kustahimili ukame na zingine zinastahimili kwenye maji mengi.

“ Tukiweza kugundua tunaweza kuongeza idadi ya mbegu na pia kuzifanyia uzalishaji au kupandikiza ili iwe na hizo tabia na Mbegu itakayopatikana itapelekwa mikoa mingine na kupandwa kulingana na hali ya hewa na mazingira ya mkoa,”amesisitiza Nnko.

Mratibu wa Utafiti wa zao la alizeti Taifa na Meneja Mradi kati ya TARI na AMDT,Frank Reuben amesema lengo la mradi ni kuongeza upatikanji wa mbegu na kuongeza usalama wa mbegu nchi.

“Tunapoongelea usalama wa mbegu ni kuhakikisha mkulima yoyote ambaye anahitaji mbegu aweze kupata mbegu bora ambayo imethibitishwa na Taasisi ya Udhibiti wa Ubora wa Mbegu(TOSC) lakini hiyo mbegu hata iwe wakati wa hali mbaya ya hewa au nzuri mkulima atapanda mbegu na kuota inaitwa usalama wa mbegu,”amefafanua.

Frank amesema Kuna uhitaji mkubwa wa mbegu za alizeti na mahitaji yanaongezeka mwaka hadi mwaka na ikipatikana mbegu tani 5,000 itafanya wakulima wengi wapate mbegu lakini ikipatikana tani 15000 itafanya wakulima wote nchini waweze kupata mbegu .

“Ili kuzalisha mbegu za kutosha AMDT inashauri ni muhimu kuwepo ubia kati ya serikali na sekta binafsi na sisi hilo tumetekeleza kiasi cha fedha tunachopata tunagawana na makampuni ya mbegu tunawajenge uwezo wa kuzalisha mbegu bora kwa kuwapa mafunzo na kufanya ufuatiliaji kuhakikisha mbegu inakidhi viwango,”ameeleza.

Aidha amesema Kwa mwaka wa kwanza walishirikisha kampuni tatu kwa mwaka huu wameshirikisha kampuni mbili na moja wapo inamilikiwa na vijana na wanategemea mwaka ujao waongeze makampuni hadi matano na kuwajenga uimara.

Amesema wanawashauri wakulima kutumia mbegu bora yenye nembo na wanawaita wakulima kuangalia mbegu katika shamba na wanatoa huduma zao kwa mashamba makubwa.

Naye Mtafiti wa TARI Ilonga,Witnesspeacequeen Kundi amesema wanafanyia utafiti wa mazao ya mikunde kuona jinsi gani zinaongeza rutuba katika udongo kupitia mazao na wanaangali ni jinis gani ya kuzalisha zao hilo na kusambaza kwa wakulima na kufanya kilimo mzunguko kwa mkulima wa alizet.

“Itamsaidia mkulima ambaye atashindwa kupata mbolea ya viwandani kipindi akivuna alizeti anaweza kupata hilo zao na zao hilo mkulima akipanda halivuni atachukua mbegu lakini majani na mshina yatabaki kwenye udogo kwaajili ya rutuba,”amefafanua.

Habari Zifananazo

Back to top button