Kodi ya majengo yapanda
MAMLAKA ya mapato Tanzania (TRA) kwa kushirikiana na shirika la umeme Tanzania (TANESCO) imeeleza kuwa serikali imefanya mabadiliko ya sheria ya serikali za mitaa ya utozaji kodi ya majengo SURA 289 kupitia sheria ya fedha ya 2023 ambapo viwango vya utozaji kodi vimebadilika pamoja na wigo wa ukusanyaji kodi hiyo umeongezeka kwa kujumuisha nyumba zilizopo maeneo ya Wilaya.
Taarifa iliyotolewa na TRA leo Julai 26, 2023 imesema moja ya mabadiliko hayo ni nyumba ya kawaida iliyokuwa ikitozwa sh 12,000 kwa mwaka sasa itatozwa sh 18,000 kwa mwaka sawa na sh 1,500 kwa mwezi.
Nyumba za ghorofa katika maeneo ya Majiji, Manispaa na Halmashauri za mji zilizokuwa zinatozwa sh 60,000 kwa kila sakafu kwa mwaka sasa zitatozwa sh 90,000 kwa mwaka sawa na sh 7,500 kwa mwezi.
Taarifa hiyo ya TRA imeongeza wamiliki wote wanaostahili kupata msamaha wa kodi ya majengo wataendelea kupata msamaha huo kwa kufuata utaratibu uliokuwepo awali.