MTWARA: MABALOZI wa Norway na Uswisi nchini Tanzania, wanatarajiwa kuhudhuria tamasha la ngome za asili za makabila yanayoishi mkoani Mtwara.
Tamasha hilo linalojulikana kama MaKuYa litafanyika Oktoba 21, 2023 katika viwanja vya Mkanaledi mjini Mtwara. Tamasha hilo limeandaliwa na Taasisi ya ADEA.
Akizungumza na waandishi wa habari Mjini Mtwara, Mkurungezi wa Taasisi hiyo Said Chilumba amesema lengo la tamasha hilo ni kukuza, kuendeleza, kuhifadhi na kutangaza utamaduni na ngoma za asili za watu wa Mtwara.
“Tamasha hili limelenga kupeleka ujumbe kwa vijana ambao wameacha asili ya kwao na kuiga asili za watu wengine, mfano vijana wasanii kuvaa hereni, nguo zisizo kuwa na heshima kwa kuiga kutoka nchi za watu Magharibi,” amesema.
Tamasha hilo litawaleta pamoja zaidi ya watu 2000 wakiwemo wasanii wa makabila ya Wamakonde, Wamakua, Wamwera na Wayao.