Mabasi yatozwa faini kupandisha nauli

MAMLAKA ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), imeyachukulia hatua mabasi 62 ikiwa ni pamoja na kuyatoza faini ya Sh 250,000 kila moja kutokana na makosa mbalimbali yakiwemo ya kuzidisha nauli kinyume nauli elekezi.

Makosa mengine ni kutotoa risiti kwa njia ya kielektroniki na kutoandika taarifa sahihi katika tiketi za abiria.

Mkurugenzi Mkuu wa LATRA, Habibu Suluo aliliambia HabariLEO kuwa mabasi hayo ni kutoka katika Kituo cha Mabasi cha Magufuli, Dar es Salaam ingawa utaratibu wa kushughulikia mabasi yanayokiuka sheria unaratibiwa nchi nzima kupitia ofisi za mamlaka hiyo.

Suluo alitolea mfano wa basi lililokamatwa kutokana na kosa la kupandisha nauli kinyume cha utaratibu ambapo badala ya nauli ya Sh 60,000 kutoka Dar es Salaam hadi Musoma, basi hilo liliwatoza abiria Sh 75,000, baada ya abiria kukataa kulipa Sh 85,000 waliyotaka awali.

“Baada ya abiria kuuliza waliambiwa basi linakaribia kujaa na nauli ni shilingi 85,000 lakini waliposema fedha hiyo hawana wakapunguziwa hadi shilingi 75,000. Tulilikamata basi hilo tukalitoza faini na kuwaamuru kurudisha nauli waliyojiongezea,” alisema.

Aliongeza kuwa baada ya kupata taarifa hiyo, basi hilo lilitozwa faini ya Sh 250,000 na kuamriwa kuwarudishia abiria wote fedha iliyozidi ambayo ni Sh 15,000 kwa kila abiria na kutoa onyo kwa wamiliki wa mabasi kuwa hatua kali zaidi zitachukuliwa ikiwa hali hiyo itaendelea.

Alisema mabasi mengine yalikamatwa kwa makosa ya kuwapa abiria tiketi ambazo sio za mfumo wa kielekroniki na kulazimika kulipa faini huku akiwakumbusha abiria kuhakikisha kuwa tiketi wanazopewa ni za kielektroniki na pia zinakuwa na maelezo yote muhimu ikiwa ni pamoja na kiwango sahihi cha pesa alicholipa.

Hivi karibuni LATRA ilitoa vibali vya ziada 452 katika mikoa mbalimbali nchini ili kukidhi matakwa ya hali ya usafiri nchini katika jitihada za kukabiliana na wingi wa abiria katika kipindi cha sikukuu za mwishoni mwa mwaka.

Hatua nyingine iliyochukuliwa alisema ni kuruhusu kampuni za mabasi kuongeza safari kutoka na kuelekea mikoani hususani katika mikoa yenye changamoto pamoja na kutoa leseni maalumu kwa ajili ya magari ya kukodi kwa watu wanaopenda kusafiri kama kikundi.

Ofisa Mfawidhi wa LATRA katika Kituo cha Mabasi cha Magufuli, Eyudi Nziku aliliambia HabariLEO kuwa kampuni zilizoongeza safari kwenda mikoani ni pamoja na Abood, Allys na nyingine zimeongeza safari kutoka Dar es Salaam kwenda Arusha, Bukoba, Mwanza na Mbeya.

Alisema vibali vilivyoongezwa vimezingatia magari yote yenye uwezo wa kubeba abiria kuanzia 42 na kuendelea yanayojumuisha mabasi ya Tata, Eicher, Yutong, Zongtong, Scania pamona na Fuso za injini ya nyuma.

Habari Zifananazo

Back to top button