Mabondia watakaovaana Moshi wapimwa afya

ZAIDI ya mabondia 10 wamejitokeza leo kupima afya zao kuelekea kwenye pambano la Kili Boxing linalotarajiwa kufanyika Februari 25, mwaka huu Moshi, Kilimanjaro.

Jopo la madaktari waliofanya tukio hilo Dar es Salaam walieleza kuwa hufanya hivyo kwa lengo la kujua afya za mabondia hao, ambapo miongoni mwa magonjwa wanayoyapima ni virusi vya ukimwi, magonjwa ya zinaa pamoja kupima ujauzito kwa upande wa wanawake.

Naye Mratibu wa Peaktime Sports, ambao ndiyo waandaji wa pambano hilo, Bakari Hatibu alisema kutakuwa na viwango vya hali ya juu siku ya mapambano hayo na kuwataka wadau mbalimbali wajitokeze kuunga mkono mchezo huo.

 

Naye bondia maarufu kwa sasa nchini, Karim Mandonga ambaye atapambana na mpinzani wake Ally Bozinia kutoka Tanga, amesema kuwa ataingia na kauli mbiu mpya iitwayo kantangaze.

Alisema amejipanga kuendeleza ushindani katika pambano hilo ambalo anaamini linasubiriwa na wadau wengi.

“Nitaonesha maajabu siku hiyo nataka kuonesha mashabiki wangu kuwa mimi ni mtu kazi kweli na ninakuja na kauli yangu mbiu mpya ya Kantangaze, wataisoma vizuri siku hiyo ya pambano,” alisema Mandonga.

Mandonga pia aliwataka mabondia wenzake wawe na nidhamu, kwani bondia anapojituma atafanikisha malengo yake na kuweza kuwa na viwango vya juu na kupata wasaa wa kushiriki mapambano mengi yatakayoendelea kumuweka juu na kumpa ujuzi wa kutosha.

 

Habari Zifananazo

Back to top button