Mabula ashauri uwepo wa maeneo ya uwekezaji
WAZIRI wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk Angeline Mabula amezitaka halmashauri zote nchini kuhakikisha zinatenga maeneo ya uwekezaji.
Dk Mabula amesema hayo leo wakati wa mkutano wa hadhara katika viwanja vya Kangae katika kata ya Nyakato wilayani Ilemela mkoani Mwanza.
Amesema maeneo ya uwekezaji yanapokuwa yametengewa na kujulikana ni ya shughuli zipi inakuwa inasaidia sana katika kuweza kuepuka migogoro isiyokuwa na ulazima.
Dk Mabula amewataka watumishi wa manispaa ya Ilemela kuhakikisha wanatatua matatizo ya ardhi pamoja na kutoa hati za ardhi kwa wakati.
Ameitaka halmashauri ya jiji la Mwanza pamoja na Manispaa ya Ilemela kuhakikisha ujenzi au ukarabati unaofanyika kwenye maeneo ya jiji la Mwanza na Manispaa hiyo inazingatia mpango kabambe wa jiji hilo.
Ameiagiza halmashauri ya jiji la Mwanza kutoa elimu kuhusiana na mpango kabambe wa jiji la Mwanza kwa wananchi wa maeneo hayo ili kuwapa uelewa na ufahamu zaidi kuhusu mpango huo kabambe.
Katika hatua nyingine,Dk Mabula amewapongeza wakazi wa kata ya Nyakato kwa kufikia hatua nzuri katika ujenzi wa shule ya msingi Kangae. Alisema Shule hiyo ikimalizika itakuwa msaada mkubwa kwa watoto wa mtaa wa Kangae na maeneo ya jirani.
Amewataka viongozi wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) wawe wanakagua miradi ya maendeleo mara kwa mara na sio kusubiria wakati wa ziara za viongozi.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela Apolinary Modest amesema watafanyia kazi maelekezo mbali mbali yaliotolewa na Dk Mabula.