WAZIRI wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk Angeline Mabula amewataka wananchi waliokabidhiwa hati miliki za ardhi wilayani Handeni mkoani Tanga kuhakikisha wanapanda miti kwenye maeneo yao ikiwa ni moja ya sharti lililopo katika hati ya ardhi.
Dk Mabula ametoa kauli hiyo leo tarehe 22 Machi 2023 wilayani Handeni wakati akikabidhi hati milki za ardhi kwa wananchi wa Halmashauri ya Mji wa Handeni.
Amesema, katika kuhakikisha maeneo wanayomilikishwa yanakuwa na utunzaji mzuri wa mazingira wizara yake imeona ije na sharti la kuwataka wanaomilikishwa kupanda miti mitano katika eneo wanalomilikishwa ili kutunza mazingira.
Kwa mujibu wa Dk Mabula, kumekuwa na tabia kwa baadhi ya wananchi hukata miti kwa visingizio vya matumizi mbalimbali jambo linalosababisha uharibifu wa mazingira katika maeneo hayo.