Mabula: Vijana hawaaminiki

MAKAMU  Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC)  Stanslaus Mabula  amesema kuwa takwimu za utoaji na urejeshwaji wa mikopo ya Halmashauri zinaonesha vijana wengi hawaaminiki katika urejeshaji kikamilifu mikopo kupitia asilimia 10 ya mapato ya ndani.

Ameyasena hayo alipoambata na Kamati ya LAAC kukagua Kikundi cha Vijana cha Zongwe fishing kinachojishughulisha na uvuvi wa samaki katika ziwa Tanganyika, kata ya Kasanga wilayani Kalambo.

Advertisement

Mabula, amesema Kikundi cha Vijana cha Zongwe fishing kilikopeshwa shilingi milioni 6.5  mwaka 2020 lakini mpaka sasa imepita miaka mitatu kikundi kimeweza kujesha shilingi 900,000  tu.

Katika halmashauri ya Kalambo vijana wamekopeshwa asilimia 30 ya mikopo, wakati wanawake wamepata asilimia 62.5, sisi vijana tumerogwa na nani? tunasubiri kukimbia mitaani kulalamika kuwa Serikali haitusaidii lakini ukweli ni kwamba tunapewa fursa hatuzitumii.” Amesema Mabula

Amesema, kutoka na sababu zilizoelezwa na kikundi kuwa nyavu zilinasa kwenye mawe pamoja na boti kuharibika.

Aidha, Mabula amemtaka Mkurugenzi kuona namna ya kukiongezea Kikundi hicho shilingi milioni moja itakayowasaidia kununua nyavu ili kuendelea na shughuli za uvuvi zitakazowawezesha kurejesha mkopo.

Aidha, Mabula amemtaka Afisa Maendeleo ya Jamii kuhakikisha anakutana na kikundi hicho na kufanya mapitio upya kwa kukagua mali za kikundi na kuwasaidia namna ya kurejesha fedha zilizosalia.

Kikundi cha Zongwe Fishing kilipata mkopo kutoka Halmashauri shilingi milioni sita na nusu mwezi Septemba 2020, baada ya kupata mkopo Kikundi kilinunua vifaa vya uvuvi ambavyo ni injini moja ya boti, boti mbili na nyavu Pc 30 za kuvulia samaki aina ya Sangara na Kuhe, madeli 3 ya kuhifadhia samaki kupata ubaridi, life jacket 5, turubai 2, boya moja na uzi wa kushonea.