Mabuye wapongeza ujenzi wa barabara

Mabuye wapongeza ujenzi wa barabara

WANAKIJI cha Mabuye wilayani Missenyi, wameipongeza Wakala wa Barabara  za Vijijini na Mijini (TARURA) kwa  hatua kubwa ya utengenezaji  wa barabara ya Mabuye- Itera  kwa kiwango cha changarawe.

Akizungumza wakati Mwenge wa Uhuru ulipofika kijijini hapo mapema leo, Almachius Alchides, ambaye ni mkazi wa kijiji hicho, alisema awali bararabara hiyo ilikuwa mbovu, jambo lililowasumbua wakati wa mavuno.

Pia alisema ilikuwa na changamoto kubwa wakati wa mvua kwa wanafunzi walipokuwa wanaenda shuleni, lakini sasa ipo vizuri.

Advertisement

Kwa upande wake kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa mwaka 2022,  Sahili Geraruma alisema ameridhishwa na matengenezo ya barabara hiyo, ambapo mbio za mwenge wa Uhuru ziliridhia kuzindua  barabara hiyo ya Mabuye-Itera yenye urefu wa kilometa 2.4

Alitoa wito kwa wananchi kuzalisha mazao yao kwa wingi, kwani hakuna kikwazo kwa sasa kinachosababisha wao kutosafirisha mazao yao na kuuza.

Pia amesema ameridhishwa na utendaji wa Tarura, kwani miradi mbalimbali iliyopitiwa na Mwenge wa Uhuru Kagera imetekelezwa katika kiwango cha kuridhisha.

Kwa mujibu wa Meneja wa Tarura, wilayani Missenyi, Ali Maziko, barabara hiyo imekamilika kwa kilometa 2.4 na lengo ni kuitengeneza kwa ubora hadi kilometa 5.5.