Machifu wahimizwa kushiriki kutatua kero
MACHIFU wametakiwa kufanya kazi kwa kushirikiana na serikali na jamii katika kutatua kero ikiwemo kukemea maovu na ukatili unaotendeka miongoni mwa familia.
Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Baraza la Machifu Mkoa wa Dodoma, Yasin Bilinje wakati wa mkutano mkuu wa uchaguzi wa machifu uliofanyika Jijini Dodoma.
Aliwataka machifu kufanya kazi kwa kushirikiana na serikali na jamii katika kutatua kero ikiwemo kukemea maovu na ukatili unaotendeka miongoni mwa familia.
“Kazi ya machifu siyo kuzurura mitaani na maofisini bali wajibu wake ni kuhakikisha wanaisaidia serikali katika kutatua kero zinazotokea kwenye familia zikiwemo za ukatili na zile za kukeketa mtoto wa kike,” alisema.
Naye Katibu wa Baraza la Machifu Mkoa wa Dodoma, Jackson Ndahani alisema nafasi ya uchifu ipo kisheria, hivyo wanatakiwa kijithamini na kujitambua ili waweze kufanya kazi zao kwa kujiamini.
Kwa upande wake, Mlezi wa Machifu mkoa wa Dodoma, Mohamed Keba aliwataka machifu kuangalia uwezekano wa kuibua miradi ili waondokane na ugumu wa uchumi unaowakabili.
Alisema pamoja na kazi waliyonayo ya kuongoza watu pia wawe na maono ya kuibua miradi yenye tija itakayowaletea mafanikio ya kiuchumi kipitia nafasi zao.
Keba ambaye pia alikuwa msimamizi wa uchaguzi wa machifu aliwataka kivunja makundi waliyokuwanayo wakati wa kugombea yuongozi, badala yake sasa wawe kitu kimoja katika kushirikiana.
Katika uchaguzi huo, nafasi ya Mwenyekiti alichaguliwa Yasin Bilinje, Makamu Jackson Tupa, Katibu Jackson Ndahani na Makamu Katibu Asher Kamwaya.