Machinga Complex tayari kutumika

MKURUGENZI wa Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru amesema soko la Machinga Complex limekamilika kwa asilimia 100 hivyo wafanyabiashara ndogondogo wanapaswa kuhamishia shughuli zao hapo.

Mafuru alisema Jumatano soko hilo lililogharimu Sh bilioni 9.5 lina uwezo wa kuchukua wafanyabiashara takribani 5,000 na kwa mwaka linatarajiwa kuingiza Sh bilioni 1.2.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari jana, Mafuru alisema kuwa soko hilo limekamilika kwa asilimia 100, limegharimu Sh bilioni  9.53 ambapo kiasi cha Sh bilioni 6.5 ni mapato ya ndani kutoka halmashauri na Sh bilioni tatu zilitolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya umaliziaji wa soko hilo baada ya kuona kazi kubwa iliyofanyika.

Alisema kuwa ifikapo Septemba 23, mwaka huu wafanyabiashara ndogondogo wanatakiwa kuhamishia biashara zao kwenye soko hilo.

“Wafanyabiashara wote wawe ndani ya soko na tarehe 24 tutafanya usafi kwenye maeneo yote ambayo wafanyabiashara wamepisha,” alisema.

Alisema soko hilo litakuwa na wafanyabiashara wa aina mbalimbali; nguo, viatu, simu, stationary, bidhaa za urembo, mafundi vyerehani, saluni za kike na kiume, wapiga picha.

“Uwezo wa soko kuchukua watu 3,000 kwa mkupuo, zitakuwepo huduma zote muhimu kama kituo cha kisasa cha polisi, eneo la kunyonyeshea watoto, vyumba vya utunzaji wa mizigo, tutaweka baa za kisasa, yenye kaunta tatu, sehemu ya mama lishe na kutakuwa na huduma za kifedha ATM na mawakala kutoka kampuni mbalimbali za simu,” alisema.

Mafuru alisema kuwa soko hilo linategemea kuingiza Sh bilioni 1.2 kwa mwaka.

Alisema kuwa mradi huo utawasaidia kupanda juu kimapato lakini pia ni eneo lenye usalama kwa ajili ya biashara kwani litawekwa kamera maalumu (CCTV) hivyo hata taasisi za kifedha zinaweza kuwapatia mikopo kwa ajili ya kukuza mitaji yao kwa kuwa wapo katika eneo rasmi.

Alisema eneo hilo la soko lina ukubwa wa mita za mraba 16,060.

“Wafanyabiashara ndogondogo wa mitaani wanatakiwa kwenda kwenye soko hilo, hatutaki kuona mfanyabiashara kapanga bidhaa kwenye maeneo yasiyoruhusiwa, wengi wanaweka bidhaa hadi nje ya majengo ya ofisi za serikali,” alisema.

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button