Machinga Iringa kuelekea soka la Mlandege

MKUU wa Wilaya ya Iringa, Veronica Kessy ametangaza kesho kuwa ni siku ya mwisho kwa machinga wote waliosalia katika maeneo yasio rasmi mjini Iringa kwenda katika soko la Machinga la Mlandege na baada ya hapo serikali itatumia mkono wake wa sheria kuwaondoa.

Hatua hiyo imekuja ikiwa ni siku kadhaa baada ya uongozi wa Shirikisho la Umoja wa Machinga Tanzania (SHIUMA) kufanikiwa kutuliza ghasia zilizokuwa zinafanywa mara kwa mara na machinga hao dhidi ya serikali.

Pamoja na kutuliza ghasia za machinga hao uongozi huo wa SHIUMA umefanikiwa kuunda uongozi wa muda wa SHIUMA Iringa mjini utakaoshirikiana na serikali na wadau kushughulikia changamoto zilizosalia baina ya machinga na serikali.

Advertisement

Katika ghasia zao za hivikaribuni mbali na kufunga kwa mawe barabara kuu za magari zinazopita jirani na soko hilo la Mlandege, wafanyabiashara hao walitangaza kurejea katikati ya mji wa Iringa katika maeneo yasio rasmi hatua waliyosema inalenga kuishinikiza halmashauri ya manispaa ya Iringa kusikiza madai yao.

Madai ya machinga hayo ambayo yalimlazimu Mkuu wa Mkoa Halima Dendego kuunda kamati na kuanza kuyafanyia kazi yalikuwa ni pamoja na kulifanya soko hilo la Mlandege ndio liwe soko la jumla la malimbichi zote kama ndizi, nyanya, viazi njegele na zinginezo zinazoingia katika masoko mbalimbali ya mjini Iringa.

Mengine ni kuwarudisha katika soko hilo machinga wote waliobaki katika maeneo yasio rasmi vikiwemo vichochoro vya mjini Iringa, huduma ya usafiri wa bajaji na daladala ipite katika soko hilo, huduma ya maji itawanywe, kuwe na mnada mmoja wa kila wiki, vifaa vya kukusanya taka na mitaji.

Ombi lao lingine katika soko hilo lililojengwa kwa ufadhili wa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Salim Asas ni pamoja na kupunguza gharama ya huduma ya choo kutoka Sh 200 hadi Sh 50 na kujenga choo kingine ili kusogeza huduma jirani zaidi na watu.

Akitangaza machinga wote waliosalia katika maeneo yasio rasmi kwenda katika soko la Mlandege katika kikao cha baraza la madiwani kilichoutambulisha uongozi wa SHIUMA Taifa na ule wa muda wa manispaa hiyo leo, Mkuu wa Wilaya alisema;”Kesho tutafanya kikao kitakachoshirikisha viongozi wa SHIUMA na machinga wote.”

Aliiagiza halmashauri ya manispaa hiyo kupita na gari la matangazo na kuwatangazia machinga wote kuhudhuria ili wakapewe maelekezo yanayowataka kwenda katika soko la Mlandege.

Baada ya kesho, Mkuu wa Wilaya alisema serikali haitakuwa na mjadala na machinga watakaoonekana wakizagazagaa na biashara zao katika maeneo yasio rasmi.

Akitoa shukrani kwa niaba ya viongozi wenzake, Mwenyekiti wa Machinga Iringa Mjini, Kessy Dandu aliomba msamaha kwa vurugu zote zilizokuwa zikifanywa na machinga huko nyuma akisema utaratibu watakaoutumia kushughulikia migogoro yao kuanzia sasa utakuwa ni ule wa kukutana na mamlaka kupitia meza ya majadiliano.

Naye Mwenyekiti wa SHIUMA Taifa, Matondo Masanja alitoa onyo kwa uongozi mpya wa machinga Iringa Mjini akisema yoyote atakeyeshiriki matukio yoyote ya machinga hao yenye muelekeo wa kuvunja amani, atakuwa amejiondoa mwenyewe na nafasi yake itajazwa na machinga wengine.

Wakati huo huo, baraza hilo limemchagua kwa kura zote July Sawani kuwa naibu meya wa manispaa hiyo kwa kipindi cha pili.

Mstahiki Meya wa Manispaa ya Iringa, Ibrahim Ngwada alimpongeza Sawani kwa kuchaguliwa kushika nafasi hiyo akimtaka kuzingatia sheria, kanuni na taratibu katika kutekeleza majukumu yake ili asivuke mipaka yake.

6 comments

Comments are closed.