MACHINGA wanaofanya biashara katika soko la Machinga la Mlandege mjini Iringa, leo wametangaza kurejea katikati ya mji katika maeneo yasio rasmi hatua waliyosema inalenga kuishinikiza Halmashauri ya Manispaa ya Iringa kusikiliza kilio chao.
Wakitangaza uamuzi huo mbele ya jeshi la Polisi na baadhi ya viongozi wa halmashauri hiyo, machinga hao wameituhumu halmashauri hiyo kushindwa kuwaondoa machinga wenzao waliorudi na kusalia katika maeneo yasio rasmi, ili waungane nao katika soko lao hilo.
Hatua hiyo imekuja baada ya machinga hao kufanya mgomo uliokwenda sambamba na kufunga barabara kuu zinazopita karibu na soko hilo na kusababisha adha kubwa kwa watumiaji wa barabara hizo.
Akizungumza Katibu wa Machinga Mkoa wa Iringa, Joseph Mwanakijiji amesema shida yao nyingine na halmashauri hiyo ni kuzuia usafiri wa bajaji kupita pembezoni mwa soko hilo la machinga hatua inayowakosesha wateja.
Uamuzi wao wa kurudi katika maeneo yasio rasmi wameufanya baada ya sharti lao la kutoongea na kiongozi mwingine yoyote nje ya Mkuu wa Mkoa kutofanikiwa kwa kile kilichoelezwa yupo jijini Mbeya kwenye maadhimisho ya wiki ya wakulima (Nanenane).
Machinga hao walishinikiza kuonana na Mkuu wa Mkoa, ili kumkabidhi soko hilo lililojengwa kwa ufadhili wa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Salim Asas kwa zaidi ya Sh Milioni 200, ili na wao warejee katika maeneo ya awali yasio rasmi ikiwemo barabara maarufu ya mjini Iringa ya Mashine Tatu.
“Kwa kuwa Mkuu wa Mkoa hayupo, msimamo wa Machinga wenzangu ni kwamba hatuwezi kumsubiri tukiwa katika soko hili, kwa hiyo na sisi tunarudi katika maeneo tuliyoondolewa hadi atakaporudi,” Mwanakijiji alisema.
Machinga hao wamesema kitendo cha wenzao kubaki katika maeneo yasio rasmi kumeendelea kuwakosesha wateja katika soko rasmi la Machinga la Mlandege na hivyo kuua mitaji yao na kuwaongezea umasikini.
Comments are closed.