Machinga sasa kutumia EFDs
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Kodi Kariakoo, umeanza kusajili wamachinga wote wanaofanya biashara katika eneo la Kariakoo kutumia Mashine za Kielektroniki (EFDs) kwa ajili ya kutoa risiti za mauzo na mwisho wa usajili huo ni Machi 30, 2023.
Mkoa huo mpaka sasa umesajili wafanyabiashara hao wadogo 5,373 na kupatiwa mashine za EFDs bure, huku lengo ni kusajili wamachinga 8,900 wanaojihusisha na biashara ndogo zenye mapato ya kuanzia sifuri hadi Sh milioni nne.
Wanaolengwa kutumia mashine hizo ni wauzaji wa mbogamboga, matunda, wauzaji wa nguo, viatu na bidhaa zilizotumika ili kuongeza uelewa wa matumizi ya mashine hizo na kuwa na utaratibu wa kutoa risiti halisi baada ya mauzo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Meneja wa TRA Kariakoo, Alex Katundu alisema wamachinga wanapatiwa mashine hizo bure na kwamba hawatakatwa kodi yoyote endapo mauzo yao kwa mwaka yatakuwa chini ya Sh milioni nne.
Alisema wamachinga hao pia wamepewa Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN), makadirio yao na kibali cha kulipa kodi ili kwenda kutafuta leseni ya biashara na wanavyoendelea kutoa risiti ndivyo wataangalia mapato yao kama wanastahili kulipa kodi au la.
“Kwa mujibu wa taarifa ya Kamishna Mkuu iliyotolewa Julai Mosi mwaka huu, ilielekeza kwamba wanaofanya biashara ndani ya eneo la Kariakoo wawe na TIN namba na mashine za EFDs bila kujali udogo au ukubwa wa biashara zao. Eneo la kikodi Kariakoo ni la kimkakati hivyo unapofanya biashara hapa lazima usajiliwe,” alisema Katundu.
Aliongeza kuwa: “Tunaendelea kuhamasisha wamachinga wote kujisajili ili kuhakikisha kwamba mfanyabiashara anayekwenda kununua bidhaa ndani ya Kariakoo, anapewa risiti kwa kitu chochote ambacho atanunua.
”
Alisema wafanyabiashara wasio waaminifu wamekuwa wakiwatumia wamachinga kukwepa kodi kwani wapo wengine barabarani ambao hawafananii na wamachinga halisi kwa kuwa kuna watu nyuma yao.
Alisema ili kuepuka ukwepaji kodi wa aina hiyo ambao hufanywa kwa makusudi, serikali iliweka mkakati huo kuhakikisha anayefanya biashara ndani ya Kariakoo awe amesajiliwa na chochote kinachouzwa hapo kiwe na risiti.
Alifafanua kuwa sababu za kutoanza kutoza kodi kwa wamachinga hao ni kuwalea ili biashara zao zikue na kisha kulipa kodi kulingana na mapato yao.
“Elimu imekuwa changamoto kwa wafanyabiashara wadogo wadogo na hata wakubwa, lakini tutaendelea kuwaelimisha ili kuhakikisha wanatambua umuhimu wa kulipa kodi halali na kwa hiari ili kukwepa adhabu za faini na riba kwa kushindwa kutoa risiti halali,” alisisitiza.
Kwa mujibu wa Katundu, Mkoa wa Kodi Kariakoo una mikakati mitatu ya kuhamasisha wafanyabiashara kutumia mashine za EFDs kutoa risiti halali na kuwaelimisha wanunuzi wa bidhaa kuhakiki risiti wanazopewa kama ni za malipo halali.
Alisema Kariakoo ni soko kubwa linalowakutanisha wafanyabiashara kutoka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Visiwa vya Comoro hivyo ni lazima kuhakikisha mapato ya serikali hayapotei kwa maendeleo ya nchi.
Alieleza kuwa wamebandika mabango mbalimbali ya kuhamasisha utoaji wa risiti ya fedha halali za mauzo kwa njia ya kielektroniki kwani kwa kushindwa kufanya hivyo faini ni kuanzia Sh milioni tatu hadi Sh milioni 4.5.
Pia alisema mtu anayenunua bidhaa na kushindwa kudai risiti halali, atatozwa faini ya kuanzia Sh 30,000 hadi Sh milioni 1.5.
“Wafanyabiashara wasikudanganye kwamba mtandao unasumbua kutoa risiti kupitia mashine ya EFDs, tatizo hawatumi ripoti ya mauzo yao kwa siku iliyopita hivyo unapotaka risiti lazima ikwame. Tunaendelea kuwahamasisha kutoa na kudai risiti halali kwa maendeleo ya nchi yetu,” alisisitiza Katundu.