Machinga watii amri ya serikali Iringa

ZOEZI la kuwaondoa machinga katika maeneo yasioruhusiwa mjini Iringa imeanza kuzaa matunda tangu izinduliwe rasmi Novemba 19, mwaka huu.

Mitaa mbalimbali ya mji wa Iringa iliyokuwa ikitumiwa na wafanyabiashara hao ipo safi (imekauka machinga hao) na watumiaji wengine waliokuwa wakishindwa kupita katika barabara zake, sasa wanapita kirahisi.

Wengi wao ambao kwa muda mrefu walikuwa wanagomea kwenda katika masoko yaliyotengwa kwa ajili yao, wametii amri hiyo ya serikali na kuleta furaha kwa Jumuiya ya Wafanyabiashara Mkoa wa Iringa iliyokuwa ikilalamila wanachama wake wenye maduka katika maeneo hayo kushindwa kufanya biashara kwa kuwa wateja wengi waliokuwa wakidakwa na wafanyabiashara hao wadogo.

Akitangaza oparesheni ya kuwaondoa wafanyabiashara holela iliyoanza Novemba 19, mwaka huu katika maeneo yasio rasmi, Mkuu wa Mkoa wa Iringa Halima Dendego alisema “itakuwa oparesheni endelevu na hatutamvumilia machinga yoyote atakayekiuka maelekezo ya serikali.”

Dengego aliwataka wafanyabiashara wote holela kutii maelekezo ya serikali yanayowataka kwenda katika maeneo rasmi yaliyotengwa kwa ajili yao ili wafanye shughuli zao kwa amani.

Alisema Rais Samia Suluhu Hassan alishatoa maelekeo kwa mikoa yote nchini kutenga maeneo maalumu kwa ajili ya machinga na kilichobaki ni utekelezaji.

Ili kuipa nguvu oparesheni hiyo, Mkuu wa Mkoa aliitisha mkutano wake na viongozi wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Mkoa wa Iringa, Umoja wa Wafanyabiashara wa Masoko na Shirikisho la umoja wa Machinga Iringa na kusisitiza wafanyabiashara hao kufanya shughuli zao katika maeneo waliyopangiwa.

Katika mkutano huo makundi hayo ya wafanyabiashara walikubali na kusaini hati ya maridhiano na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa inayowata kwenda katika maeneo waliyotengewa.

Kwa kusaini hati hiyo mmoja wa madiwani ha halmashauri hiyo Hamid Mbata alisema; “Hatutarajii tena kuwaona machinga katika maeneo yasio rasmi.”

Machinga hao wanatakiwa kwenda katika masoko yao ya Mlandege makaburini, Zizi, Kitanzini na Ngome.

Pamoja na kutii amri hiyo ya serikali baadhi ya machinga wameomba waruhusiwe mida ya jioni kutandaza bidhaa zao pembezoni mwa barabara ya soko la Malandege Makaburini ili kuwavuta wateja wanaopita katika njia hiyo.

Mwisho.

Habari Zifananazo

Back to top button