Machinjio ya Sh bilioni 29 yazinduliwa Mvomero

MACHINJIO ya kisasa ya Nguru Hills Ranch Ltd imezinduliwa rasmi mjini Mvomero ambapo inauwezo wa kuchinja ng’ombe 100 na mbuzi 1000 kwa siku.

Mradi huo wenye thamni ya Sh bilioni 29 (Dola milioni 15) ni uwekezaji wa ubia kati ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), Eclipse Investment (LLC) kutoka nchini Oman na Kampuni ya Busara Innvestiment (LLP).

Akizundua machinjio hayo Waziri Ndaki amesema uwekezaji wa miradi ya machinjio ya kisasa ya mifugo ni kutafsiri dhamira ya serikali kupambana na umaskini kwa kutoa ajira kwa watanzania na wafugaji kupata soko la uhakika la mifugo yao katika kuwainua kiuchumi.

Waziri Ndaki ametaja dhamira nyingine ni kuongeza mapato ya serikali ya kodi mbalimbali na kuleta fedha za kigeni kutokana na mauzo ya nyama kwenye masoko ya nchi za nje.

“Wanapotokea wawekezaji kwenye sekta hii tafsiri uwekezaji wao unakwenda kuwainua wafugaji na wakulima ambao ndio kundi kubwa la watanzania, hivyo nawapongeza PSSSF na wabia wenzake kwa kugusa kundi kubwa la watanzania” amesema Ndaki

Waziri Ndaki amewakata wawekezaji hao kuzingatia viwango na ubora vinavyotakiwa katika soko la nje ili kuleta ushindani kwa vile mahitaji ya nyama nje ya nchi ni makubwa tofauti na kinachozalishwa.

Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF Hosea Kashimba amesema machinjio yanamilikiwa kwa ubia na wanahisa watatu ambao ni Eclipse Investiment (LLC) yenye hisa asilimia 46 , PSSSF wenye hisa asilimia 39 na Kampuni ya Busara Innvestiment (LLP) yenye hisa asilimia 15.

Kashimba amesema soko la nyama inayozalishwa kwenye mashinchinjo hayo imepata soko la nje ya nchi kwa asilimia 80 zikiwemo za mashariki ya kati hasa ya Oman ,na asilimia 20 kwa ajili ya soko la ndani .

Amesema fedha hizo zilitumika kununua mashine na mitambo, kukarabati jengo la kiwanda, ujenzi wa mabwawa ya kutibu majitaka, ujenzi wa barabara ya kuingia kiwandani na gharama za uendeshaji.

Kashimba amesema ,wanahisa wamewekeza jumla ya dola za kimarekeni milioni 10 na kati hizo, PSSSF imewekeza dola milioni 3.9 na hivyo kiufanya kuwa na asilimia 39 za hisa wakati dola milioni tano ikiwa ni mkopo kutoka Benki ya Azania.

Amesema mradi una miundombinu muhimu ikiwemo eneo la malisho lenye ukubwa hekta 2, 328, eneo lenye uwezo wa kuchukua Ng’ombe 10,000 na Mbuzi 15,000 kwa wakati mmoja, na miundombinu ya maji inayohusisha visima vitano yenye uwezo wa kuzalisha lita 20,000 kwa saa.

Mradi huo ulianza mwaka 2018 lakini ugonjwa wa Covid -19 uliponza ulisababisha mashine zilizoangizwa kutoka nje kuchelewa kuletwa wakiwemo na wataalamu wake hadi kufikia Julai mwaka 2021 zilipoletwa na kufungwa.

“ Mradi huu pia utaongeza kipato cha wakulima,kwa kununua mazao ambayo yatatumika kutengeneza chakula cha mifugo kwa ajili ya kunenepesha mifugo kabla ya kuchinja” amesema Kashimba.

 

Habari Zifananazo

Back to top button