Macho, masikio kwa Rais Samia leo

RAIS Samia Suluhu Hassan leo anaratajiwa kuwa mgeni rasmi katika sherehe za maadhimisho ya Siku ya wafanyakazi (Mei Mosi) kitaifa katika uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa jana alieleza kuridhishwa na maandalizi ya sherehe hizo.

Majaliwa alisema taarifa alizopewa na Waziri wa Nchi katika Ofisi yake anayeshughulikia Kazi, Vijana , Ajira na Wenye Ulemavu, Profesa Joyce Ndalichako , Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Fatma Mwassa na Rais wa Shirikishio la Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Tumaini Nyamhokya maandalizi yamekwenda vizuri.

“Tunamtarajia wakati wowote hapa Morogoro (Rais Samia), jambo hili ni sio la kubahatisha, jambo hili ni jambo muhimu na kwa kuwa mkuu wa nchi ndiye anakuja hapa maandalizi yetu lazima yafanane na ukubwa wa mgeni wetu rasmi” alisema Majaliwa baada ya kukagua uwanja wa Jamhuri na akaongeza;

“Lakini hapa mwenyekiti wa shirikisho ametuambia maandalizi ya mwaka huu ni makubwa zaidi kuliko mwaka jana. Sherehe hizi ni muhimu na ni siku moja pekee  ambazo zinafanyika mara moja kwa mwaka na wafanyakazi wanakaa pamoja leo ( Mei Mosi , 2023)”

Alikipongeza chama kilichoanda na  vyama vyote vya  wafanyakazi kwa kushiriki kikamilifu katika maandalizi hayo kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Ofisi ya Waziri Mkuu na wadau wengine.

Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Tumaini Nyamhokya alimweleza Majaliwa kuwa vyama vya wafanyakazi vimejipanga kuwa na idadi ya kutosha ya wafanyakazi katika maadhimisho hayo.

Miongoni mwa mambo ambayo wafanyakazi wanatarajia Rais Samia Suluhu Hassan kuyazungumza ni maboresho zaidi ya maslahi ya wafanyakazi ikiwamo mishahara na uondoaji wa vikwazo vya ustawi wao.

Hivi karibuni serikali ilisema bungeni Dodoma kuwa utumishi wa umma ni nguzo muhimu katika uendeshaji na uendelezaji wa nchi na umeendelea kutoa mchango ulioiwezesha Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zenye uchumi wa kipato cha kati cha kiwango cha chini.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene alisema hayo wakati anawasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka wa fedha 2023/2024.

Simbachawene alisema serikali ina matarajio makubwa kuwa mchango wa watumishi wa umma katika maendeleo utaendelea kuiwezesha nchi kufikia uchumi wa kati wa kiwango cha juu.

Aliwaeleza wabunge kuwa maendeleo hayo yanatarajiwa kuongezeka kwa kuimarisha uchumi shindani na viwanda kwa maendeleo ya watu kama inavyobaishwa katika Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano Awamu ya Tatu.

Simbachawene alisema hadi mwezi uliopita serikali imelipa Sh bilioni 25.7 ambazo ni madai ya malimbikizo ya mishahara kwa watumishi 14,398.

Pia alisema serikali imelipa Sh bilioni 8.5 ambazo ni madai ya malimbikizo ya mishahara kwa watumishi 2,942 waliokoma utumishi.

Simbachawene alisema katika kipindi cha mwaka mmoja kuanzia Februari mwaka juzi hadi mwezi uliopita serikali imelipa madai ya malimbikizo ya mishahara kwa watumishi 119,098 yenye thamani ya Sh bilioni 204.4

Pia alisema imetoa vibali vya ajira mpya 30,000 na vibali vya ajira mbadala 7,721 kwa waajiri kutoka katika taasisi mbalimbali.

Habari Zifananazo

Back to top button