TIMU ya Macklion FC imetwaa kwa mara ya tatu mfululizo ubingwa wa mashindano ya Kombe la Chemchem baada ya kuitandika Macedonia FC mabao 2-0 katika mchezo wa fainali uliopigwa uwanja wa Mdori uliopo wilayani Babati mkoani Manyara.
Jumla ya timu 33 zilishiriki michuano hiyo yenye lengo la kupiga vita ujangili wa twiga katika eneo la vijiji 10 ambavyo vinaunda Hifadhi ya Jamii ya Wanyamapori ya Burunge mkoani Manyara.
Michuano hiyo pia imehusisha timu za vijana ambapo Maweni FC imetangazwa mabingwa kwa walio na umri wa chini ya miaka 18 baada ya kuisambaratisha Mwada mabao 2-0.
Kwa Upande wa timu za Wasichana Mwada Queens ilitwaa Ubingwa kwa mara ya kwanza baada ya kuichapa mabao 4-0 Maweni Queens .
Akifunga mashindano hayo afisa michezo Mkoa wa Manyara, Pastory Samwel kwa niaba ya Katibu Tawala Mkoa Arusha, amewapongeza wandaaji wa mashindano hayo taasisi ya Chemchem kwa kutoa elimu ya uhifadhi kupitia michezo lakini pia kupambana kuhakikisha Soka linaendelea kuchezwa.
Alieleza mashindano hayo chini ya kauli mbiu ya ‘Okoa Twiga’ imekuwa ni daraja kwa vijana kuweza kutimiza ndoto zao kwani wapo ambao wamepita hapo na sasa wanacheza Ligi Kuu akiwemo kiungo wa Ihefu FC,Yusuph Athumani.
“Afcon ya mwaka 2027 itachezwa hapa Tanzania na Mkoa wa Arusha mechi zitachezwa hivyo kwetu itakuwa ni fursa kwa uwanja wetu huu bora wa Mdori kupata nafasi ya timu kufanyia mazoezi.” aliongeza Samwel.
Kwa upande wake mkurugenzi wa taasisi ya Chemchem,Nicolaus Negri alisema wametumia zaidi ya Sh milioni 99 kuendesha mashindano hayo ambapo pia wamefanikiwa kutoa elimu juu ya uhifadhi wa wanyamapori katika eneo la Hifadhi ya Jamii ya Burunge.
“Dhumuni letu ilikuwa ni kuhamasisha utunzaji wa mazingira,kutoa elimu kwa jamii juu ya uhifadhi wa mazingira,kupiga vita ujangili wa wanyamapori,kujenga mahusiano katika jamii pamoja na kuibua vipaji”,amesema Negri.
Kwa upande wa zawadi timu ya Soka kwa wakubwa bingwa amepata Sh milioni 2.5 mshindi wa pili Sh milioni 1.5 ,mshindi wa tatu Sh milioni 1 Wanawake bingwa Sh milioni 1.5 mshindi wa pili Sh milioni 1 mshindi wa tatu Sh 500,000.
Vijana chini ya umri wa miaka 18, bingwa Sh milioni 1 mshindi wa pili Sh 600,000,mshindi wa tatu Sh 400,000 pia kulikuwa na zawadi za medali,kiatu cha dhahabu kwa mfungaji na mchezaji bora lakini pia Gloves za dhahabu kwa kipa bora.
Ofisa Wanyamapori wilaya ya Babati,Laizer alisema Halmashauri ya Wilaya ya Babati inapongeza chemchem kutumia michezo katika kupambana na ujangili.