HOSPITALI ya Rufaa ya Kanda Mbeya (MZRH), imepokea madaktari bingwa wanne kutoka Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China, ambao wanatarajiwa kutoa huduma mbalimbali za kibobezi, ikiwemo za upasuaji kwa kushirikiana na madaktari wa hospitali hiyo.
Akizungumza ofisini kwake mapema leo, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya, Dk Godlove Mbwanji, amewashukuru na kuwakaribisha wataalamu hao na kuishukuru Serikali ya China kwa kuendelea kuimarisha ushirikiano wa Tanzania na China katika sekta ya afya.
“Madaktari hao watatoa huduma mbalimbali za kitabibu kwa wagonjwa mahututi, utoaji salama wa dawa za usingizi na ganzi pamoja matibabu ya upasuaji wa watoto na upasuaji wa mifupa,” amesema Dk Godlove Mbwanji.
Kwa upande wake kiongozi wa kundi hilo la madaktari kutoka China, Dk Dubinbing, ameushukuru uongozi wa MZRH kwa mapokezi mazuri na kuahidi kutoa ushirikiano mzuri kwa wataalam wa hospitali katika kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi wa Tanzania.