Madaktari bingwa waanza upasuaji Kitete

KAMBI maalumu ya madaktari bingwa kutoka Hospitali za Rufaa za Mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Dodoma imeanza kufanya upasuaji kwa wagonjwa waliokutwa na uhitaji wa huduma hiyo katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora Kitete.

Hayo yamesemwa leo na kiongozi wa madakatri hao ambaye pia ni Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Pwani, Tumbi, Dk Amani Malima na kwamba kazi hiyo ilianza Jumatatu na itadumu kwa siku tano.

Amesema siku ya kwanza walianza kuwaona wagonjwa na kuwachambua na kwa wale waliohitaji upasuaji, wameanza huduma hiyo Jumanne katika idara ya mifupa, masikio, pua na koo pamoja na matumbo.

“Jana tulifanya upasuaji kwa watoto wenye matatizo ya masikio, koo na pua pamoja na matumbo, kwa hiyo leo tunaendelea kwa upande wa idara ya mifupa hususani kwa  watoto wenye matatizo ya mifupa ambayo wamezaliwa nayo.

“Pia kuna watu waliopata ajali lakini wamekuwa na ulemavu ambao unaweza kurekebishika, hivyo tupo hapa kwa nia ya kuwahudumia,” alisema.

Dk Malima amesema lengo kubwa  la kambi hiyo ni kutoa huduma za matibabu ya kibingwa wa wananchi wa mkoa wa Tabora na kuwapunguzia  gharama za kuzifuata huduma hizo nje ya mkoa, kwani wananchi wengi wamekuwa wakifuata huduma  Dar es Salaam, Mwanza, Kilimanjaro na Dodoma.

“Serikali yetu kupitia kwa Rais Dk  Samia Suluhu Hassan imekua ikifanya vizuri na mambo makubwa katika sekta ya afya, hivi sasa kuna maboresho ya miundombinu yakiwemo majengo na ununuzi wa vifaa tiba, hivyo tumewaleta madaktari mabingwa hawa, ili kuweza kutoa huduma hizi kwa fani mbalimbali.

“Sisi kama wataalamu wa hospitali za rufaa za mikoa tumeona ni vyema kujiongeza licha ya kuwapunguzia gharama Watanzania wa kuzifuata huduma hizi nje ya Tabora, lakini tutawajengea pia uwezo wataalamu wa hospitali hii, ili kuhakikisha wananchi wa hapa wanaendelea kupata huduma kama hizi, hivyo tumeunda kikundi cha madaktari bingwa kutoka fani mbalimbali zaidi ya 20”.

Amewaomba wafanyabiashara, kampuni na watu wenye uwezo wajitokeze kusapoti huduma kama hizo kwenye maeneo yao waliyozaliwa, ili kuweza kuwasaidia wananchi katika huduma za afya.

Habari Zifananazo

Back to top button