Madaktari bingwa waja kivingine Mwanza

TIMU ya madaktari bingwa imepiga kambi ya siku tano, kuanzia leo hadi Desemba 9, 2022 katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Sekou Toure, ili kusogeza huduma karibu na wananchi.

Timu inaundwa na madaktari bingwa wenyeji wa kambi  na wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda, Bugando, kwa huduma za magonjwa ya watoto, macho, meno, mama na uzazi pamoja na mionzi.

“Mengine ni magonjwa ya damu, mfumo wa chakula, akili, kusafisha damu na maabara pamoja na dawa,” amesema Katibu Tawala wa Mkoa (RAS), Balandya Elikana, wakati wa uzinduzi wa kambi leo Desemba 5, 2022.

Amepongeza wanajamii kujitokeza, akasema mkoa utasogeza huduma wilaya zote na mikoa jirani ya kanda ya ziwa, kwa utaratibu huo wa kambi.

Kuhusu gharama, Mganga Mfawaidhi Sekou Toure, Bahati Msaki, amesema wagonjwa wenye uwezo watachangia gharama na wengine watahudumiwa kwa msamaha kupitia kitengo cha ustawi wa jamii.

Mabingwa pia wanatoa elimu kwa umma juu ya magonjwa mbalimbali, visababishi na jinsi ya kujikinga.

Daktari bingwa wa magonjwa ya damu, Gloria Mapunda, ameelimisha kwamba tatizo la seli mundu bado ni kubwa, kwani tafiti zinaonesha kila mwaka takribani watoto 11, 000 nchini wanazaliwa na tatizo hilo.

“Linachangia asilimia saba ya vifo vya watoto chini ya miaka mitano. Ni la kurithi na linazuilika, hasa wachumba wanapopata vipimo kabla ya kutafuta watoto,” amesema.

Habari Zifananazo

Back to top button