Madaktari JKCI watoa tiba za kibingwa Malawi

MADAKTARI Bingwa wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) wametoa matibabu ya kibingwa kwa wagonjwa zaidi ya 724 wa moyo nchini Malawi walikoweka kambi ya siku tano.

Matibabu hayo yamefanikiwa chini ya uratibu wa Kamati ya Utalii Tiba inayoongozwa na Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Dk Mohamed Janabi na Makamu wake, Abdulmalik Mollel ambaye ni Mkurugenzi wa Global Education Link (GEL).

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) baada ya kuwasili Dar es Salaam jana, kiongozi wa msafara wa madaktari hao ambaye ni daktari bingwa wa maradhi ya Moyo wa JKCI, Dk Angela Muhyoza alisema kambi hiyo ilifanyika katika Hospitali ya Qeen Elizabeth.

Advertisement

Dk Muhyoza alisema walikuwa na madaktari bingwa wa watoto wawili na madaktari bingwa wa watu wazima wawili na wataalamu wengine waliokuwa wakiwasaidia.

Alisema kati ya wagonjwa waliowahudumia, 524 waligundulika kuwa na matatizo ya moyo ambapo baadhi yao walipatiwa tiba hapohapo wakati wagonjwa 200 walihitaji huduma za upasuaji mkubwa wa kufungua kifua.

“Miongoni mwa wagonjwa hao, 60 wanahitaji matibabu ya haraka kutokana na matatizo waliyonayo kwa hiyo wasipopata matibabu ndani ya muda huo wanaweza kupata matatizo zaidi, wananchi wa Malawi wamefurahia huduma zetu na walitamani tuendelee kuwepo nchini kwao,” alisema Dk Muhyoza.

Wakati huo huo, Serikali ya Malawi imeishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuwapeleka wataalamu wa moyo kwa ajili ya kufanya uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo kwa wananchi wa nchi hiyo.

Waziri wa Afya nchini Malawi, Khumbize Chiponda alitoa shukurani hizo alipotembelea Hospitali ya Queen Elizabeth kuangalia huduma zilizokuwa zikitolewa na wataalam wa afya kutoka JKCI wakati wa kambi ya siku tano ya matibabu ya moyo.

Khumbize alisema Malawi na Tanzania wamekubaliana kuwa na kushirikiano katika kujengeana uwezo kwani nchi hiyo bado haijaweza kuanzisha hospitali ya moyo, hivyo kupitia kambi hiyo wataenda kujitathimini uwezo wao kama wanaweza kuanzisha kituo ambacho kitakuwa kinatoa huduma za matibabu ya kibingwa ya moyo nchini humo.

“Ndugu zetu Watanzania wapo mbele yetu katika kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo kwa sababu yatari wameshafungua taasisi ambayo inatoa huduma za moyo na imewekeza wataalamu na vifaa vya kutosha, naamini tukiendelea kupata ujuzi kama huu nasi tutaweza kufungua hospitali ya moyo,” alisema Khumbize

Khumbize alisema matibabu ya moyo ni ya gharama, hadi sasa Malawi ina wagonjwa zaidi ya 500 wenye magonjwa ya moyo wanaosubiria kuwapeleka nje ya Malawi kwa ajili ya matibabu.

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo kwa Watoto kutoka JKCI, Parvina Kazaura alisema katika kambi hiyo walifanya uchunguzi na matibabu ya moyo kwa watu wazima na watoto na kila siku watoto zaidi ya 80 wamekuwa wakifanyiwa uchunguzi wa moyo.

“Kwa bahati mbaya, watoto wengi wenye magonjwa ya moyo ya kuzaliwa nayo wamekuja wakiwa na umri mkubwa ambapo ilipaswa kufanyiwa upasuaji mapema baada ya kuzaliwa lakini hawakufanyiwa kutokana na huduma hizi kutokuwepo hapa Malawi,”alisema.