Madaktari MOI wafanya tathmini huduma Mtwara

Madaktari MOI wafanya tathmini huduma Mtwara

JOPO la madaktari bingwa wabobezi sita kutoka Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI), wamefika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini, mkoani Mtwara kufanya tathmini ya kina, ili kuanza kutoa huduma za upasuaji wa mifupa na mishipa ya fahamu hospitalini hapo.

Wakiongozwa na daktari bingwa  wa upasuaji magonjwa ya ubongo, uti wa mgongo na mishipa ya fahamu, Dk. Hamisi Shabani, amesema wametumwa na Wizara ya Afya kutembelea hospitali hiyo, ili kufanya tathimi na kubaini mambo mbalimbali yanayohitajika kabla ya kuanza huduma hizo bobezi.

“Jopo hili la wataalamu limetumwa na Wizara ya Afya kupitia Taasis ya Mifupa MOI kuja kufanya tathmini ya kina hospitalini hapa (Hospitali ya Rufaa Kanda ya Kusini), kuweza kuangalia namna gani hizi huduma bobezi kwenye upasuaji wa mifupa pamoja na mishipa ya fahamu, ianze hapa,” amesema Kaimu Mkurungenzi wa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Kusini, Dk Habati Masigati.

Advertisement

Amesema madaktari hao wametumia takribani siku tatu kufanya tathmini hiyo, ambapo wamepita kila kitengo hospitalini hapo, kwa kushirikiana na wataalamu wengine hospitalini kubaini aina mbalimbali ya vifaa vilivyopo, utendeji kazi wake, maeneo ya kutolea huduma pamoja na  vyumba vya upasuaji na maeneo ya kulaza wagonjwa.

Masigati amesema madaktari hao bingwa wabobezi, baada ya kufanya tathmini wanatarajiwa kupeleka ripoti katika ngazi mbalimbali za maamuzi mpaka kufika wizarani.