Madaktari waagizwa kutunza siri za wagonjwa

WAZIRI wa Afya, Ummy Mwalimu amewataka wauguzi na madaktari kutoa huduma za afya kwa weledi na kuzingatia miiko na maadili ya taaluma huku wakielezwa kupunguza semina zinazo wafanya washindwe kuonekana vituoni.

Pia wataalamu wanatakiwa kutotoa siri za wagonjwa kwani kuna mtu imeonekana imetolewa siri baada ya kulazwa hospitalini  hivyo mganga mkuu wa mkoa afuatilie suala hilo nani alitoa siri hiyo.

Waziri Ummy  alisema hayo jana mkoani Shinyanga  wakati akizungumza na watumishi wa huduma za afya  katika ziara yake ya kukagua utoaji wa huduma bora kwa wateja au wagonjwa.

Advertisement

Waziri Ummy alisema si maadili ya kitaaluma daktari au mtoa huduma ya yoyote kutoa siri za mgonjwa, na kubainisha kuwa watakao endelea kukiuka miiko ya utoaji huduma za afya watasimamishiwa  na kututiwa leseni zao.

“Hapa naangalia kwenye mitandao ya kijamii naona kuna taarifa ya mwanume kuwa amejikata uume kwamba hataweza kufanya mapenzi tena, nimemuagiza mganga mkuu alifuatilie hilo nani katoa taarifa ya Mgonjwa,”alisema Waziri Ummy

Waziri Ummy aliwasihi madaktari na watoa huduma za afya kuendelea kutumia lugha nzuri kuhudumia wagonjwa na kuwahi maeneo yao ya kazi kwa wakati.

Watumishi wa afya punguzeni  semina na makongamano ya mara kwa mara,bali wajikite zaidi kuhudumia wananchi na kuimarisha afya zao.

Katika hatua nyingine aliwataka Wafamansia wafanye maoteo sahihi ya dawa, ili upatikanaji wa dawa uwepo kwa wananchi, na siyo kuwepo na dawa kwenye Makaratasi lakini uhalisia  hakuna dawa.

Aliwaagiza wakurugenzi wa halmashauri, kuajiri wataalamu wa afya wa mkataba kupitia fedha za mapato ya ndani, ili kupunguza tatizo la upungufu wa tumishi katika sekta ya afya,wakati serikali ikiendelea kutatua tatizo hilo.

Alisema Rais Samia ametoa fedha nyingi kuboresha huduma za afya, pamoja na upatikanaji wa vifaa tiba na vitendanishi, lakini baadhi ya vifaa tiba vinashindwa kutumika kutokana na upungufu wa wataalamu.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dk Yudas Ndugile, akisoma taarifa ya huduma za afya mkoani humo, alisema upatikanaji wa huduma umeimarishwa pamoja na upatikaji wa dawa asilimia 89.9.

Dk Ndugile alisema  licha ya huduma hizo kuboreshwa, lakini bado wanakabiliwa na tatizo la upungufu wa watumishi na madaktari bingwa katika Hospitali ya Rufani mkoani humo, pamoja na magari ya kubeba wagonjwa.

Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Johari Samizi akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Christina Mndeme, alimpongeza Rais Samia kwa kutoa Sh  billioni 26 kwenye sekta ya afya mkoani  hapa na kuahidi maelekezo ambayo ameyatoa waziri watayatekeleza.

3 comments

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *