Madaktari waandaa mashindano ya riadha

MADAKTARI wa hospitali mbalimbali nchini, pamoja na wananchi wengine wanatarajiwa kushiriki mashindano ya riadha yaitwayo Doctors Marathon Julai 15, mwaka huu.
Mgeni rasmi katika mashindano hayo atakuwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na mashindano hayo yatafanyika katika Viwanja vya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili(MUHAS).
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Rais wa MAT, Dk Deus Ngilana amesema lengo la mbio hizo ni kununua vifaa tiba vya dharura katika Hospitali za Wilaya za Mikoa ya Lindi, Katavi na Simiyu.
Dk Ngilana amebainisha kuwa lengo lingine ni kuhamasisha wananchi kufanya mazoezi, ili kuepukana na magonjwa yasiyoambukiza.
Lengo lingine aliloainisha ni kuamsha ari ya watu kuwa na bima za afya, kwani kati ya watu milioni 60 asilimia 15 ndo wana bima na wengine asilimi 85 hawana.
“Tumeamua kukimbia kwa sababu tunataka kuonesha jamii yale ambayo tunayowashauri wakati wa kliniki tunakuja kuwaambia hadharani kwamba ni kizuri na ni moja ya njia ya kupambana na magonjwa yasiyoambukiza,”alisisitiza.
Amesema kumekuwa na magonjwa yasiyoambukiza kama kisukari,presha,satani na mengi na mfuko wa Bima wa Taifa unaelemewa.
Amesema wananchi watakaojitokeza kushiriki wataweza kupima afya zao ikiwemo shinikizo la damu, sukari na uzito.
“Huu ujumbe tunataka uwafikie madaktari wote na Watanzania tunataka tukutane katika mazingira ya furaha, tufanye mazoezi tutengeneza nafasi nzuri kati ya madaktari na watu wanaowahudumia, hii ni agenda ya taifa ndo maana tunashirikisha viongozi wakubwa,” amebainisha.