Madaktari waanza mgomo Kenya

MADAKTARI nchini Kenya wameanza mgomo wa wiki moja kutokana na serikali kuchelewesha kupeleka wahudumu wa afya. Pia wanalalamikia mazingira duni ya kazi wanayosema wanapaswa kufanyia kazi, Shirika la Habari BBC linaripoti.

Awali Mahakama ya Kazi ilitoa amri ya kusitisha hatua ya kiviwanda ili kutoa nafasi ya mazungumzo. Jaji alimtaka Waziri wa Kazi kufanya mazungumzo na chama cha madaktari na waajiri siku ya Alhamisi kutafuta suluhu.

Lakini muungano huo unasema haukupata agizo la mahakama.

Kenya inakabiliwa na mzozo wa afya kwa wananchi wake. Huku madaktari katika vituo vya matibabu vya serikali wakigoma, wagonjwa wanaohitaji msaada imeripotiwa kuwa watateseka.

Zaidi ya wanafunzi 1,000 wa udaktari ambao wamemaliza mafunzo yao na wanahitaji kufanya kazi kwa mwaka mmoja kabla ya kupata leseni zao hawajaanza kazi tangu Januari.

Katika taarifa hiyo ya BBC imeeleza kuwa Wizara ya Afya nchini humo haina pesa za kutosha kuwalipa.

Machi 4 mwaka huu, mtandao wa habari CITIZEN nchini Kenya ulichapisha taarifa kuwa madaktari walitoa notisi ya mgomo wa siku saba kuanzia wiki hii.

Muungano wa Madaktari na Madaktari wa Meno (KMPDU) Jumatatu ulifanya maandamano ya amani jijini Nairobi, kupinga miongoni mwa mambo mengine ikiwemo kupigwa risasi kwa Katibu Mkuu wao Davji Atellah.

Madaktari walisisitiza msukumo wao kwa Waziri wa Afya, Susan Nakhumicha kuwaajiri wafanyakazi hao, wakisema kuchelewa kufanya hivyo kumeathiri huduma katika hospitali za umma kote nchini.

Habari Zifananazo

Back to top button