Madaktari wagoma wakidai mazingira bora ya kazi

Madaktari wagoma wakidai mazingira bora ya kazi

MADAKTARI katika sehemu mbalimbali za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) wameendelea na mgomo wao hata baada ya serikali kuwasihi warudi kazini.

Chama cha Madaktari nchini (SYNAMED) kimeitaka serikali kuharakisha mkutano na madaktari hao kikisema wagonjwa wanaendelea kuumia kutokana na maamuzi ya serikali yasiyoridhisha.

Mgomo huo ambao ulianza miezi kadhaa ingawa haukuwa wa moja kwa moja una lengo la kudai mazingira bora ya kazi na kuheshimu ahadi zilizotolewa na serikali za kuongeza mishahara yao ambapo madaktari walianzisha kaulimbiu ya ‘hospitali bila madaktari’.

Advertisement

Katika hospitali kuu ya mji mkuu Kinshasa, vitanda katika vyumba kadhaa vya matibabu vimejaa wagonjwa. Madaktari wachache waliopo hufanya kazi kwa mzunguko na kuchukua zamu kwa karibu miezi miwili kufanya huduma hiyo.

“Wagonjwa wanaolazwa hospitalini wanahudumiwa na wakuu wa idara na wakuu wa huduma. Sisi, SYNAMED hatupokei wagonjwa tena,” alieleza Dk Aime Umba, mmoja wa wasimamizi wa chama hicho cha madaktari akiwa katika hospitali kubwa ya umma katika Jiji la Kinshasa.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa chama cha wafanyakazi, Dk Fabien Nzoko, aliinyooshea kidole serikali kwa kuhusika na hali hiyo. “Ni serikali inayotakiwa kuwajongelea watu wake ambao ni madaktari na kuwasikiliza kwani wananchi wanapata tabu sana. Serikali ndio inahusika na kile kinachotokea kwa raia wa DRC,” aliongeza Nzoko.

Alisema kama serikali ingefanyia kazi yale makubaliano ya Agosti 3 mwaka huu juu ya kuboreshwa kwa mazingira ya kazi na maslahi kwa madaktari leo kusingekuwa na mgomo huo na kuisihi serikali isiweke pamba masikio yake kwa kuwa inaumiza wananchi wa Congo.

 

 

 

/* */