JAMII imetakiwa kuacha kuwanywesha watoto pombe kwani ina athari kubwa kwa kundi hilo.
Rai hiyo imetolewa ikiwa ni siku chache baada ya kuwapo taarifa za watu waliolazwa kutokana na kunywa pombe ya kienyeji iliyosadikiwa kuwa na sumu, miongoni mwao wakiwamo watoto wadogo.
Watoto watatu wenye umri chini ya miaka mitano ni miongoni mwa watu 53 waliolazwa katika Hospitali ya Wilaya Vwawa, kutokana na kunywa pombe ya kienyeji aina ya komoni yenye sumu.
Akizungumza na HabariLEO juu ya tukio hilo, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Vwawa, Keneth Lesilwa aliliambia HabariLEO kwamba katika wilaya hiyo, hasa vijijini, wapo wazazi wengi na walezi wanapokunywa pombe, huwanywesha watoto wadogo pombe ya kienyeji pasipo kujua madhara yake.
“Katika tukio la juzi la watu kulazwa hospitalini kutokana na kunywa pombe yenye sumu, inashangaza miongoni mwao wapo watoto wadogo chini ya miaka mitano nao wamenyweshwa pombe ya kienyeji,” alisema.
Aliongeza: “Hii inaonesha kuwa kuna wazazi wengi wanaowanywesha watoto pombe. Tulibaini mtoto wa mwaka mmoja na miezi 11, mwingine miaka miwili na mwezi mmoja na mtoto wa miaka mitatu.
”
Kuhusu wagonjwa waliofikishwa hospitali kwa ajili ya unywaji pombe hiyo alisema wote wametibiwa na kuruhusiwa baada ya afya zao kuimarika.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa hospitali binafsi ya Ilas, Frederick Ngoi alisema madhara ya unywaji pombe kwa watoto wadogo ni pamoja na kuathiri maini, figo, kuathiri ukuaji wa mtoto na kusababisha ulaji hafifu kwa watoto.
Alisema pombe ni sumu hivyo huathiri moja kwa moja ukuaji wa mtoto kwa kuathiri ufanyaji kazi wa figo na maini ya watoto.
Dk Ngoi alisema madhara mengine makubwa kwa mtoto mdogo kunyweshwa pombe ni kudumaa kwa akili na mwili kwa sababu viungo vyake vinakuwa havina uwezo wa kuhimili vilevi jambo ambalo ni hatari.
“Ndiyo maana wanasema wenye umri wa chini ya miaka 18 wasinywe pombe kutokana na sumu iliyopo kwenye pombe, mtu mzima anayekunywa sana pia huathiriwa na kushindwa kula, kwa mtoto kuna madhara makubwa zaidi,” alisema Dk Ngoi.
Mkoa wa Songwe ni miongoni mwa mikoa ambayo udumavu uko juu kwa asilimia 43.
23. Sababu zinazotajwa ni pamoja na kutozingatia ulaji bora wa makundi matano ya vyakula.