Madaktari wasisitiza miguu vifundo, matege yanatibika

MOROGORO; CHAMA cha Madaktari Bingwa wa Mifupa Tanzania (TOA), kimetoa wito kwa jamii yenye watoto wenye matatizo ya viungo na miguu vifundo, wasiwafiche ndani bali wawafikishe hospitali kwa vile utaalamu upo kuwasaidia kukaa vizuri.

Rais wa chama hicho, Dk Felix Mrita alisema hayo wakati akizungumza na HabariLEO jana baada ya kuhitimisha kambi ya siku mbili ya huduma bingwa zilizotolewa na madaktari bingwa wa chama hicho mkoani Morogoro kwa kushirikiana na hospitali ya rufaa ya mkoa.

Watu 520 walionwa na kati yao, 150 walikuwa waliopata matatizo ya kuvunjika na wakawa wameunga miguu yao vibaya . Wengine ni wenye magonjwa yanayotokana na utu uzima kama vile magoti na mgongo ambao kati yao, watu 18 walifanyiwa upasuaji.

Advertisement

Alisema oparesheni hizo nyingi ni za mivunjiko ambayo miguu iliunga vibaya. Alisema wahusika wangepata huduma stahiki siku ya kwanza walipovunjika, miguu ingekaa sawa kuliko kusubiri iunge kisha ivunjwe na kuipanga tena.

Dk Mrita alisema watoto wengi waliopokewa walikuwa na changamoto ya miguu kifundo au nyayo zilizopinda ambao ni aina ya ulemavu unaotokana na matatizo ya mifupa. Alisema miguu kifundo si kitu kipya bali ni matatizo yaliyokuwapo tangu zamani.

“Hata ukiangalia watu wa zamani utawakuta miguu kama umejikunja , walikuwa wakivaa viatu na kufunga kamba lakini miguu umejikunja unaangalia juu,” alisema.

Dk Mrita alitaja kundi lingine ni la watoto wenye matege ambayo kwa sasa yanatibika. Alisema huwatokea watoto kutokana na ukosefu wa vitamini D na wakipatiwa wanakuwa sawa .

“Wengine si shida ya vitamini D bali ni maumbile yao na hawa wakifanyiwa upasuaji miguu yao inakaa sawa na opereshani nyingi za watoto matibabu yake ni bure,” alisema.

Dk Mrita alishauri akinamama wenye watoto kujenga tabia ya kuwatoa nje asubuhi ili wapate mwanga wa juaakisema ndilo suluhisho la mwanzo.

“Vitamini D ni mwanga wa jua la asubuhi, wenye watoto tunawashauri kuhakikisha wanapata huo mwanga wa jua na hii ndiyo suluhisho la mwanzo kabisa, labda endapo mtoto atakuwa na shida nyingine,“ alisema.

Dk Mrita alisema ukosefu wa vitamini D pia unawapata watu wazima hususani wanaoingia maofisini asubuhi na wanatoka usiku na hawakutani na jua.

“Kukosa hiyo dalili zake hautaweza kupata matege bali utakuwa na maumivu ya viungo, mara mgongo unafanyiwa X-Ray hakionekani kitu lakini ukipata mwanga si lazima wa jua, mwanga pekee inatosha kabisa,” alisisitiza Dk Mrita.