SERIKALI itaendelea kutekeleza mkakati wa kitaifa wa kukuza na kuendeleza kisomo na elimu kwa umma kwa kuanzisha madarasa 1,000 kwa ajili ya elimu ya watu wazima.
Waziri wa wizara hiyo, Profesa Adolf Mkenda amesema hayo bungeni Dodoma wakati anawasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya fedha katika mwaka wa fedha 2023/24.
Aidha, Profesa Mkenda alisema serikali itaendelea kutoa mafunzo ya kuwajengea ujuzi vijana 12,000 kupitia Mpango wa elimu changamani kwa walio nje ya shule awamu ya pili (IPOSA).
Aliwaeleza wabunge kuwa serikali itafanya ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa Mwongozo wa Kuwarejesha Shuleni Wanafunzi Waliokatisha Masomo katika Elimu ya Msingi na Sekondari kwa sababu mbalimbali kwa lengo la kubaini changamoto za utekelezaji wake.
Alisema serikali itachapa moduli 18 za masomo kwa hatua ya I na II kwa ajili ya vituo 151 vya elimu ya sekondari kwa njia mbadala ili kuongeza fursa za upatikanaji na mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji.
Serikali imewezesha kuwarejesha wanafunzi 1,967 (wanawake 1,046 na wanaume 86) katika Mfumo Rasmi wa Elimu.
Vilevile, imedahili jumla ya wanafunzi 23,263 (wanawake 15,006 na wanaume 8,257) katika mikoa 26 ambao wanapata Elimu ya Sekondari kwa Njia Mbadala (Alternative Education Pathway).
Pia serikali imeandaa moduli 12 za Mafunzo Endelevu kwa Walimu Kazini (Mewaka) wa Elimu ya Awali na Msingi na imetoa mafunzo kwa walimu 26,657 wanaofundisha elimu ya awali na msingi kupitia vituo vya walimu na shule teule;
imetoa mafunzo kuhusu Elimu ya Stadi za Maisha zinazolenga afya ya uzazi, VVU na Ukimwi na Jinsia kwa walimu 25,700 kati ya walimu 27,750 wa shule 18 za msingi na sekondari waliolengwa ili kuwajengea uwezo wa kufundisha masuala mtambuka.
Vilevile, imetoa mafunzo kuhusu darasa jumuishi kwa walimu 17,800 kati ya walimu 20,000 waliolengwa wanaofundisha Darasa la I – IV. Mafunzo yalilenga kuimarisha utekelezaji wa mitaala.