MADEREVA bajaji 132 wa mjini Iringa wameanza mafunzo ya udereva yatakayowawezesha kupata leseni za kuendesha vyombo hivyo vya moto baada ya Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa Daudi Yassin kuahidi kubeba gharama zake.
Mafunzo hayo yaliyoanza leo na yatakayofanyika kwa wiki moja katika ukumbi wa CCM Mkoa wa Iringa yanayotolewa na Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi (Veta) kwa kushirikiana na kikosi cha usalama barabarani Iringa.
Mwenyekiti wa Bajaji Iringa, Melabu Kiwele alisema kati ya washiriki hao wanaoendesha vyombo hivyo vya moto bila mafunzo na leseni, wanne ni wanawake.
Kiwele alimshukuru Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa akisema bila ufadhili wake huo madereva hao wanaoendesha vyombo hivyo vya moto wasingepata mafunzo hayo na leseni ya udereva ambayo gharama yake kwa kila moja ni Sh 85,000.
Akifungua mafunzo hayo Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa Allan Bukumbi alisema; “Nafarijika kuwaona vijana ambao kwa dhati mmedhamiria kuondokana na udereva wa mazoea na kwenda kwenye udereva wa kitaaluma.”
Alisema ni muhimu kwa madereva hao kujengewa uwezo ili wapate ujuzi utakaowawezesha kuondokana na kadhia za ajali za barabarani kwa kuwa watakuwa na maarifa yatakayowafanya waachane na udereva wa papara, kwani watakuwa wakizingatia sheria na alama za barabarani.
Awali Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Iringa, Mosi Ndozero aliwataka madereva hao kuzingatia yote watakayojifunza ili waifanye kazi hiyo kwa weledi katika kudhibiti ajali za barabarani.
“Ninyi ni vijana, mchango wenu unahitajika sana katika maendeleo ya Taifa hili kwahiyo ni muhimu mkakumbuka kutathimini aina ya udereva wenu katika kukabiliana na majanga ya ajali ambayo wahanga wake wakubwa ni vijana wenyewe,” alisema.
Naye Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Paulo Walalaze aliwataka madereva hao kushirikiana na mamlaka hiyo kuhakikisha mizigo wanayopewa ili kuisafirisha katika bajaji zao inakuwa na risiti za EFD.
Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Iringa Aggrey Tonga aliwataka madereva hao kuiheshimu na kuipa hadhi yake kazi hiyo akisema ni ajira inayochochea maendeleo yao.
Mwakilishi wa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, Nguvu Chengula alisema CCM itaendelea kushirikiana na madereva hao na kuhakikisha inatatua changamoto zao kwa kadri fursa itakapopatikana.