Madereva wa mabasi waonywa

NAIBU Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi (Uchukuzi), Atupele Mwakibete amesema kuwa dereva yoyote atakayeshusha abiria njiani wakati eneo hilo kuna kituo cha kushusha na kupakia abiria, hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.

Mawakibete amebainisha hayo leo Alhamisi Juni 15, 2023, alipokuwa anajibu swali la nyongeza la Mbunge wa Igunga, Nicholas Ngasa lililohoji Serikali inatoa kauli gani  kwa magari yanayoshusha abiria njiani, ili kuepusha adha kwa wananchi.

“Kama kuna basi lolote linashusha abiria njiani na wakati eneo hilo kuna kituo cha mabasi kwa mujibu wa sheria ya usalama barabarani kifungu cha 50 cha kwanza kimeeleza wazi   dereva huyo achukuliwe hatua za kisheria hivyo kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi tutaendelea kusimamia jambo hilo,” amesema Mwakibete.

Mwakibete amebainisha kuwa  mabasi yote ya masafa marefu, hupangiwa ratiba na  Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA),  ambazo  ndani yake huonesha stendi za kushusha na kupakia abiria.

“Mabasi ya masafa marefu yamepangiwa kusimama katika stendi moja tu katika kila mkoa, isipokuwa kama basi hilo lina abiria anayeshuka katika stendi ya wilaya na utaratibu huo umepangwa ili kuondoa usumbufu wa ucheleweshaji wa abiria wa masafa marefu,” amesema Mwakibete.

Habari Zifananazo

Back to top button