Madereva watakaofaulisha abiria kukiona

DAR ES SALAAM: MAMLAKA ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imesema madereva wanaofaulisha abiria kutoka chombo kimoja kwenda kingine watakapobainika watanyanganywa leseni na kuhamishwa njia wanayopita

Mkurugenzi wa Udhibiti wa Usafiri wa Barabara LATRA ,Johansen Kahatano amesema hayo leo Septemba 8, 2023 jijini Dar es Salaam wakati akitoa taarifa ya kurejeshwa kwa ratiba ya mabasi 38 ya kampuni ya New Force kuanza safari muda wa saa 9:00 usiku na saa 11:00 alfajiri.

Kuhusu ufaulishaji wa abiria amesema Mamlaka hiyo inafuatilia kwa karibu suala hilo na kuwataka wananchi kutoa taarifa ili hatua ziweze kuchukuliwa.

“Tumebaini yapo mabasi yanayotoa huduma kwenda Kahama lakini wakipakia abiria na kuwaambia wanakwenda huko lakini wanapofika eneo  la Tinde hushushwa na kutakiwa kutafuta usafiri mwingine,” amesema Kahatano na kuongeza kuwa wenye matukio hayo wapo kadhaa,wakibainika leseni zao zitanyangwanywa na kuhamishwa njia wanayoitoa huduma.

Amesema wananchi wanaofanyiwa vitendo hivyo watoe taarifa kwa Mamlaka hiyo kwa kutumia namba ya Simu 0800110019 ambayo ni ya bure na kueleza alikuwa anakwenda wapi na kashushiwa wapi.

Kahatano amesema jambo hilo ni kero kwa abiria na usumbufu,hivyo wanafuatilia na kuchua hatua.

Aidha, amesema kuna baadhi ya madereva wa mabasi yaendayo mikoani ambao hawatumii alama ya kitambulisho wakati wakitoa huduma na kuhimiza  kutumia.

Amesema  pia wamiliki wa mabasi  wahakikishe wanawahimiza madereva kutumia alama hizo za utambulisho Ili kutambuliwa katika mfumo.

Kuhusu mabasi ya New force amesema Mamlaka hiyo ilisitisha  ratiba za mabasi hayo kuanza safari muda wa saa 9:00 usiku na saa 11:00 alfajiri  kutokana na ukiukwaji wa masharti ya leseni za usafirishaji hasa kutoka kabla ya muda ulioidhinishwa,mwendokasi na matukio ya ajali za mfululizo.

Amesema Mamlaka ilitoa melekezo kwa mabasi hayo kuanza safari muda wa saa 12:00asubuhi, kutafuta mshauri mwelekezi kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa uongozi wa kampuni kuhusianana masuala ya usalama na kuwa na mpangokazi wa matengenezo ya mabasi na usimamizi wa masharti ya leseni za usafirishaji wa abiria na kutoa mafunzo kwa madereva wote kuhusu sheria za barabarani na udereva wa kujihami na kudhibiti uchovu.

Amesema baada ya kupewa adhabu hiyo LATRA ilishirikiana na Jeshi la Polisi na mshauri mwelekezi katika  kufuatilia utekelezaji wa maagizo hayo na Mamlaka imejiridhisha kampuni kutekeleza yaliyotakiwa.

Amesema kwa sababu hiyo Mamlaka imeamua kurejeshwa ratiba na leseni kwa mabasi yote 38 kuanzia Septemba 11,2023 na kuonya kuwa kutolewa Kwa ruhusa hiyo iwe ni fundisho Kwa kampuni na wasafirishaji wote wanaokiuka sheria na taratibu za usalama barabarani.

Meneja wa Kampuni ya mabasi hayo, Masumbuko Masike amekiri kuhakikisha marereva wao kuzingatiwa taratibu zote zinazotakiwa.

Habari Zifananazo

Back to top button