TUME ya Madini imejiridhisha kuwa vitu vinavyozalishwa na wawekezaji hapa nchini vina ubora unaotakiwa. Aidha, imeahidi kutoa elimu kwa wenye viwanda na kampuni kununua vya hapa nchini badala ya kuagiza nje ya nchi.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Ukaguzi na Biashara kutoka katika tume hiyo, Andrew Mgaya baada ya kutembelea kiwanda cha Max Steel kinachozalisha nyaya zinazoshikilia ukuta wa chini wa migodi na bidhaa nyingine, kilichopo Vingunguti, Dar es Salaam.
“Vitu vinavyozalishwa vina ubora, kwa kuona huku nasi tutawashauri wadau wetu kuwa vitu vingi vinavyotafutwa nje ya nchi vipo hapa Tanzania. Tunawaomba wadau wetu waje wavione. “Nimewataka watu wa Max Steel wasiishie kwa watu wa tume ya madini tu, waende kwenye taasisi tumizi, makampuni, wazabuni wanaosambaza vitu, taasisi za serikali kwa sababu hivi vitu sio vya migodini tu.
Hata watu binafsi na wa nje wanavitumia. “Kwa hiyo waende huko kwa watu wanaotumia ili waweze kujua hivi vitu vinavyotolewa kwenye taasisi ya Max Steel,” alisema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda hicho, Kishan Suchak alisema lengo lao ni kutoa huduma zinazokidhi vigezo na miongozo ya kiusalama katika madini, mafuta na gesi, ujenzi, usafirishaji wa nishati, mawasiliano na kilimo.
“Katika nyanja zote hizi tunahusika kutoa huduma kuanzia upembuzi na ujenzi, yaani mwanzo wa mradi mpaka mwisho.
“Lengo ni kuhakikisha kuwa katika nyanja zote hizo zinazalishwa hapa nchini, zinazalishwa na wazawa kwani asilimia 90 katika sekta nilizogusia zimekuwa zikiingizwa nchini kutoka China, Uturuki au Afrika Kusini,” alisema. Ikiwa ni pamoja na kuwajengea uwezo wazawa lakini pia ni kutengeneza ajira kwa wazawa.