MADIWANI wa Halmashauri ya Jiji la Arusha, wamemjia juu Mbunge wa Arusha Mjini, Mrisho Gambo na kudai tuhuma dhidi yao kwamba wamepewa viwanja vya bure katika mradi wa Bondeni City zina nia ya kuwachafua
Madiwani hao wakizungumza kwa nyakati tofauti, wamesema kuwa kitendo cha Gambo kudai wameruhusu fedha za jijini kutoka bila utaratibu, ni kauli iliyowadhalilisha, hivyo wamemba hatua kali za kinidhamu ndani ya CCM na serikali zichukuliwe dhidi yake.
Diwani wa Kata ya Baraa, Jacob Mollel, ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Fedha na Utawala, alidai tuhuma za Gambo ni za uongo, uzushi na zenye lengo la kujitafutia umaarufu kwani hakuna fedha ya halmashauri inalipwa bila kamati hiyo kuidhinisha na kwenda katika Baraza la Madiwani na Gambo ni mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo.
Diwani huyo alisema mradi wa Bondeni City, ulipitishwa kikao cha Baraza la Madiwani Novemba 22 mwaka huu kwa kupiga kura na hakuna diwani aliyepinga kati ya madiwani 33 waliohudhuria kikao hicho, hivyo maamuzi yalikuwa halali kwa mujibu wa taratibu za vikao.
Alisema madai kuwa madiwani wamepewa viwanja katika eneo hilo sio ya kweli na kama diwani amepewa basi alipewa kama mtu mwingine na sio kivuli cha udiwani kama anavyodai.
Diwani wa Kata ya Ngarenaro, Issaya Doita, ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya fedha na Utawala, alisema kauli ya Gambo ni sawa na kujisema mwenyewe kwa kuwa yeye ni mjumbe wa Baraza la Madiwani na Mjumbe wa Kamati ya Fedha na Utawala, kauli ambayo pia ilizungumzwa na Diwani wa Kata ya Lemara, Naboth Silasile, aliyesema Mbunge huyo ameamua kuwazushia uwongo.